Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 1:20-30

1 Wakorintho 1:20-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Yu wapi basi, mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa sheria? Naye bingwa wa mabishano wa nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu. Maana, kadiri ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri. Wayahudi wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima; lakini sisi tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa watu wa mataifa ni upumbavu; lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu kuliko nguvu za binadamu. Ndugu, kumbukeni wakati mlipoitwa: Wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka la juu. Ndiyo kusema, Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili awaaibishe wenye nguvu. Mungu ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana. Basi, hakuna mtu awezaye kujivunia chochote mbele ya Mungu. Mungu mwenyewe ndiye aliyewaunganisha nyinyi na Kristo Yesu. Mungu amemfanya Kristo awe hekima yetu; kwa njia yake sisi tunapatanishwa na Mungu, tunakuwa watu wake Mungu na kukombolewa.