Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 29:10-20

1 Mambo ya Nyakati 29:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Ndipo Daudi akamtukuza Mwenyezi-Mungu mbele ya mkutano wote, akisema: “Utukuzwe milele na milele, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yetu Israeli. Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote. Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. “Lakini, mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kukupa kitu? Kwa maana vitu vyote vyatoka kwako, tumekutolea vilivyo vyako wewe mwenyewe. Sisi tu wageni mbele yako, na wasafiri kama walivyokuwa babu zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli kipitacho, hapa hakuna tumaini la kukaa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wingi wote huu tuliotoa ili kukujengea nyumba kwa ajili ya utukufu wa jina lako takatifu, watoka mkononi mwako na yote ni yako. Ninajua Mungu wangu, kwamba wewe waujaribu moyo, nawe unapendezwa na unyofu. Nami, katika unyofu wa moyo wangu nimetoa vitu hivi vyote kwa hiari yangu, na sasa ninaona watu wako walioko hapa, wakikutolea kwa hiari na furaha. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, babu zetu, dumisha maazimio ya namna hiyo na fikira za namna hiyo mioyoni mwa watu wako, na ielekeze mioyo ya watu wako kwako. Mjalie Solomoni mwanangu ili kwa moyo wote ashike amri zako, maamuzi na maagizo yako, atekeleze yote ili aweze kuijenga nyumba hii ya enzi niliyoifanyia matayarisho.” Kisha, mfalme Daudi aliwaambia wote waliokusanyika, “Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Na wote waliokusanyika wakamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakamsujudia na kumwabudu Mwenyezi-Mungu na kumtolea mfalme Daudi heshima.

1 Mambo ya Nyakati 29:10-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na ushindi, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. Kwani sisi tu wageni na wapitaji mbele zako, kama walivyokuwa baba zetu wote; siku zetu duniani ni kama kivuli, na hakuna tumaini la kuishi. Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yote inatoka mkononi mwako, na yote ni yako wewe. Nami ninajua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao. Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulidumishe jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako; naye Sulemani mwanangu, umjalie ili kwa moyo wote, azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba. Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainamisha vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye.

1 Mambo ya Nyakati 29:10-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. Kwani sisi tu wageni mbele zako, na wasafiri, kama walivyokuwa baba zetu wote; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana. Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe. Nami najua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao. Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulilinde jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako; naye Sulemani mwanangu, umpe moyo mkamilifu, ili azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba. Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainama vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye.

1 Mambo ya Nyakati 29:10-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Daudi akamhimidi BWANA mbele ya kusanyiko lote, akisema: “Uhimidiwe wewe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, tangu milele hata milele. Ukuu na uweza, ni vyako, Ee BWANA, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee BWANA, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote. Utajiri na heshima vyatoka kwako; wewe ndiwe utawalaye vitu vyote. Mikononi mwako kuna nguvu na uweza ili kuinua na kuwapa wote nguvu, Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu Jina lako tukufu. “Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vitokavyo mkononi mwako. Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini. Ee BWANA Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako. Ninajua, Mungu wangu, kwamba wewe huujaribu moyo na unapendezwa na unyofu. Vitu hivi vyote nimetoa kwa hiari na kwa moyo mnyofu. Nami sasa nimeona kwa furaha jinsi watu wako walioko hapa kwa hiari yao walivyokutolea wewe. Ee BWANA, Mungu wa baba zetu Abrahamu, Isaki na Israeli, weka shauku hii ndani ya mioyo ya watu wako daima na uifanye mioyo yao iwe na uaminifu kwako. Nawe umpe mwanangu Solomoni kujitolea kwako kwa moyo wote ili kuzishika amri zako, masharti yako, maagizo yako na kufanya kila kitu ili kujenga Hekalu hili la fahari ambalo kwa ajili yake nimetoa.” Ndipo Daudi akaliambia kusanyiko lote, “Mhimidini BWANA Mungu wenu.” Hivyo wote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao. Wakasujudu na kuanguka kifudifudi mbele za BWANA na mfalme.

1 Mambo ya Nyakati 29:10-20

1 Mambo ya Nyakati 29:10-20 BHN1 Mambo ya Nyakati 29:10-20 BHN
Shirikisha
Soma Sura Nzima