1 Mambo ya Nyakati 22:1-19
1 Mambo ya Nyakati 22:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi Daudi akasema, “Hapa ndipo mahali ambapo nyumba ya Mwenyezi-Mungu itakuwa, na hii ndiyo madhabahu ambapo watu wa Israeli watatolea sadaka ya kuteketezwa.” Daudi akatoa amri wageni waliokuwa wanaishi katika nchi ya Israeli wakusanyike, naye akawapangia kazi. Akaweka waashi wachonge vizuri mawe ya kujenga nyumba ya Mungu. Daudi pia akaweka akiba tele ya chuma cha kutengenezea misumari na mafungo ya malango ya nyumba, na akiba tele ya shaba isiyopimika. Mbao za mierezi ambazo Daudi aliletewa na Wasidoni na Watiro zilikuwa hazihesabiki. Daudi akajisemea, “Nyumba ambayo mwanangu Solomoni atamjengea Mwenyezi-Mungu itakuwa ya fahari sana, ya kusifika na tukufu duniani kote. Lakini kwa vile yeye bado angali kijana na bado hana uzoefu mwingi, afadhali nimfanyie matayarisho.” Hivyo basi, Daudi akaweka akiba kubwa sana ya vitu vya ujenzi kabla hajafariki. Ndipo Daudi akamwita Solomoni mwanawe, akamwagiza amjengee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli nyumba. Daudi akamwambia Solomoni, “Mwanangu, nilikusudia moyoni mwangu kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nyumba ili kumtukuza. Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Wewe umemwaga damu nyingi kwa kupigana vita vikubwa. Kwa sababu ya damu nyingi ambayo umemwaga mbele yangu hapa duniani, hutanijengea nyumba. Hata hivyo, utapata mwana, ambaye atatawala kwa amani kwa sababu nitampa amani na maadui zake wote wa jirani. Jina lake litakuwa Solomoni, kwa maana katika siku za utawala wake, atailetea Israeli amani na utulivu. Hivyo, yeye ndiye atakayenijengea nyumba. Atakuwa mwanangu nami nitakuwa baba yake, na wazawa wake wataitawala Israeli milele.’ Sasa mwanangu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe ili ufaulu kumjengea nyumba kama alivyosema. Mwenyezi-Mungu akupe busara na akili ili atakapokupa uongozi juu ya Israeli, uzishike sheria zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Ukiwa mwangalifu, na ukizitii amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya Israeli, utastawi. Jipe moyo, uwe imara. Usiogope wala usifadhaike. Kwa juhudi kubwa, nimeiwekea akiba nyumba ya Mwenyezi-Mungu, talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na idadi isiyopimika ya shaba na chuma, kwani ni nyingi sana. Nimeandaa mbao na mawe tayari. Lakini huna budi kuongezea. Unao wafanyakazi wengi: Kuna wachonga mawe, waashi, maseremala na mafundi wa kila aina wenye ujuzi mwingi; wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma. Haya! Anza kazi! Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe!” Zaidi ya hayo, Daudi aliwaamuru viongozi wote wa Waisraeli wamsaidie Solomoni mwanawe, akisema, “Je, Mwenyezi-Mungu Mungu wenu hayuko pamoja nanyi? Je, hajawapa amani katika pande zote? Yeye aliwatia wakazi wa nchi hii mikononi mwangu na sasa wako chini ya Mwenyezi-Mungu na watu wake. Sasa, mtumikieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa nia na moyo wote. Shime basi! Mjengeeni Mwenyezi-Mungu mahali patakatifu ili sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu pamoja na vyombo vyote vitakatifu vitumiwavyo katika ibada, viwekwe ndani ya nyumba iliyojengwa kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.”
1 Mambo ya Nyakati 22:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Daudi akasema, Hii ndiyo nyumba ya BWANA Mungu, na hii ndiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Israeli. Basi Daudi akaamuru wakusanyike wageni waliokuwa katika nchi ya Israeli; akaweka waashi wachonge mawe ili kujenga nyumba ya Mungu. Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyoweza kupimika; na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro walimletea Daudi mierezi tele. Daudi akasema, Sulemani mwanangu angali ni mchanga bado, na hana uzoefu, nayo nyumba atakayojengewa BWANA haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa. Ndipo akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza amjengee BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba. Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wangu. Lakini neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu; tazama, utapata mwana, atakayekuwa mtu wa amani; nami nitampa amani mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu siku zake; huyo ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu; naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa babaye; nami nitakiimarisha milele kiti cha ufalme wake juu ya Israeli. Sasa mwanangu, BWANA na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya BWANA, Mungu wako, kama alivyonena kuhusu habari zako. BWANA na akupe busara na akili, akakuagizie juu ya Israeli; ili uishike Torati ya BWANA, Mungu wako. Ndipo utakapofanikiwa, ukiangalia kuzitenda amri, na hukumu, BWANA alizomwagizia Musa juu ya Israeli; uwe hodari, na wa moyo mkuu; usiogope wala usifadhaike. Basi sasa, tazama, katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya BWANA, talanta laki moja za dhahabu, na talanta milioni moja za fedha; na shaba na chuma isiyo na uzani; kwa vile zilivyo tele; miti tena na mawe nimeweka akiba, nawe utaweza kuongeza. Tena kwako kuna mafundi wengi, wenye kuchonga na kufanya kazi ya mawe na miti, na kila aliye stadi kwa kazi yoyote; ya dhahabu, ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, hapana hesabu; basi inuka ushike kazi, naye BWANA na awe pamoja nawe. Tena Daudi akawaamuru viongozi wote wa Israeli, kwamba wamsaidie Sulemani mwanawe, akisema, Je! Si BWANA, Mungu wenu, aliye pamoja nanyi? Na kuwapa amani pande zote? Kwa kuwa wenyeji wa nchi amewatia mkononi mwangu; nayo nchi imetiishwa mbele za BWANA, na mbele ya watu wake. Basi sasa jitieni moyo na nia kumtafuta BWANA, Mungu wenu; inukeni basi, mkamjengee BWANA Mungu mahali patakatifu, ili kulileta sanduku la Agano la BWANA, na vyombo vitakatifu vya Mungu, ndani ya nyumba itakayojengwa kwa ajili ya jina la BWANA.
1 Mambo ya Nyakati 22:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Daudi akasema, Hii ndiyo nyumba ya BWANA Mungu, na hii ndiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa Israeli. Basi Daudi akaamuru wakusanyike wageni waliokuwa katika nchi ya Israeli; akaweka waashi wachonge mawe ili kujenga nyumba ya Mungu. Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyo na uzani; na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro wakamletea Daudi mierezi tele. Daudi akasema, Sulemani mwanangu akali ni mchanga bado, na mwororo, nayo nyumba atakayojengewa BWANA haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa. Ndipo akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza amjengee BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba. Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wangu. Lakini neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu; tazama, utazaliwa mwana, atakayekuwa mtu wa kustarehe; nami nitamstarehesha mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu siku zake; huyo ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu; naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa babaye; nami nitakifanya imara milele kiti cha ufalme wake juu ya Israeli. Sasa mwanangu, BWANA na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya BWANA, Mungu wako, kama alivyonena kwa habari zako. BWANA na akupe busara na akili, akakuagizie juu ya Israeli; ili uishike torati ya BWANA, Mungu wako. Ndipo utakapofanikiwa, ukiangalia kuzitenda amri, na hukumu, BWANA alizomwagizia Musa juu ya Israeli; uwe hodari, na wa moyo mkuu; usiogope wala usifadhaike. Basi sasa, tazama, katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya BWANA, talanta elfu mia za dhahabu, na talanta elfu elfu za fedha; na shaba na chuma isiyo na uzani; kwa vile zilivyo tele; miti tena na mawe nimeweka akiba, nawe utaweza kuongeza. Tena kwako kuna mafundi wengi, wenye kuchonga na kufanyiza kazi ya mawe na miti, na kila aliye mstadi kwa kazi yo yote; ya dhahabu, ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, hapana hesabu; basi inuka ushike kazi, naye BWANA na awe pamoja nawe. Tena Daudi akawaamuru wakuu wote wa Israeli, kwamba wamsaidie Sulemani mwanawe, akisema, Je! Si BWANA, Mungu wenu, aliye pamoja nanyi? Na kuwastarehesha pande zote? Kwa kuwa wenyeji wa nchi amewatia mkononi mwangu; nayo nchi imetiishwa mbele za BWANA, na mbele ya watu wake. Basi sasa jitieni moyo na nia kumtafuta BWANA, Mungu wenu; inukeni basi, mkamjengee BWANA Mungu mahali patakatifu, ili kulileta sanduku la agano la BWANA, na vyombo vitakatifu vya Mungu, ndani ya nyumba itakayojengwa kwa ajili ya jina la BWANA.
1 Mambo ya Nyakati 22:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Daudi akasema, “Nyumba ya BWANA Mungu itakuwa mahali hapa, pia pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Israeli.” Kwa hiyo Daudi akatoa amri wakusanyike wageni wote waliokuwa wanaishi Israeli, na kutoka miongoni mwao akaweka waashi ili kuchonga mawe kwa ajili ya kujenga nyumba ya Mungu. Daudi akatoa chuma tele ili kutengenezea misumari kwa ajili ya mafungo ya malango ya nyumba na shaba tele isiyopimika. Pia akatoa magogo ya mierezi yasiyohesabika, kwa kuwa Wasidoni na Watiro walikuwa wamemletea Daudi idadi kubwa ya mierezi. Daudi akasema, “Mwanangu Solomoni bado ni mdogo wa umri na hana uzoefu. Nyumba itakayojengwa kwa ajili ya BWANA inatakiwa iwe yenye uzuri mwingi na sifa na fahari mbele ya mataifa yote. Kwa hiyo nitaifanyia matayarisho.” Daudi akafanya matayarisho makubwa kabla ya kifo chake. Kisha akamwita Solomoni mwanawe akamwagiza kujenga nyumba kwa ajili ya BWANA, Mungu wa Israeli. Daudi akamwambia Solomoni: “Mwanangu, nilikuwa na jambo hili ndani ya moyo wangu kujenga nyumba kwa ajili ya Jina la BWANA Mungu wangu. Lakini neno hili la BWANA likanijia, kusema: ‘Wewe umemwaga damu nyingi na kupigana vita vingi. Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu. Lakini utakuwa na mwana ambaye atakuwa mtu wa amani na utulivu nami nitampa utulivu mbele ya adui zake wote pande zote. Jina lake ataitwa Solomoni, nami nitawapa Israeli amani na utulivu wakati wa utawala wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu. Yeye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. Nami nitakifanya imara kiti chake cha enzi cha utawala wake katika Israeli milele.’ “Sasa, mwanangu, BWANA awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya BWANA Mungu wako, kama alivyosema utafanya. BWANA na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika sheria ya BWANA Mungu wako. Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria BWANA alizompa Mose kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa. “Nimejitaabisha sana ili kupata mahitaji kwa ajili ya Hekalu la BWANA: talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na kiasi kisichopimika cha shaba na chuma, pia mbao na mawe. Nawe waweza kuviongeza. Unao wafanyakazi wengi: Wachonga mawe, waashi na maseremala, pamoja na watu walio na ustadi katika kila kazi wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma, mafundi wasiohesabika. Sasa basi anza kazi hii, naye BWANA awe pamoja nawe.” Kisha Daudi akawaamuru viongozi wote wa Israeli wamsaidie Solomoni mwanawe. Akawaambia, “Je, BWANA Mungu wenu si yuko pamoja na ninyi? Pia si amewapa raha pande zote? Kwa maana amewatia wenyeji wa nchi mkononi mwangu, nayo nchi iko chini ya BWANA na watu wake. Sasa itoeni mioyo yenu na nafsi zenu katika kumtafuta BWANA Mungu wenu. Anzeni kujenga Maskani ya BWANA Mungu, ili mweze kulileta Sanduku la Agano la BWANA na vyombo vitakatifu vya Mungu katika Hekalu litakalojengwa kwa ajili ya Jina la BWANA.”