Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 21:1-30

1 Mambo ya Nyakati 21:1-30 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Shetani akainuka dhidi ya Israeli na kumshawishi Daudi ahesabu watu wa Israeli. Kwa hiyo Daudi akamwambia Yoabu na majemadari wa jeshi, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli kuanzia Beer-Sheba mpaka Dani. Kisha nileteeni taarifa ili kwamba niweze kufahamu wako wangapi.” Yoabu akajibu, “BWANA na aongeze jeshi lake mara mia na zaidi. Mfalme bwana wangu, kwani hawa wote si raiya wa bwana wangu? Kwa nini bwana wangu unataka kufanya hivi? Kwa nini kuleta hatia juu ya Israeli?” Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu; kwa hiyo Yoabu akaondoka na kuzunguka Israeli yote kisha akarudi Yerusalemu. Yoabu akampa Daudi jumla ya idadi ya watu wanaoweza kupigana. Katika Israeli kulikuwa na watu 1,100,000 ambao wangeweza kutumia upanga na katika Yuda watu 470,000. Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. Amri hii ilikuwa mbaya machoni pa Mungu pia; hivyo akaiadhibu Israeli. Kisha Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Sasa, ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.” BWANA akamwambia Gadi, mwonaji wa Daudi, “Nenda ukamwambie Daudi, hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ” Kwa hiyo Gadi akamwendea Daudi akamwambia, “Hili ndilo BWANA asemalo: ‘Chagua: miaka mitatu ya njaa, au miezi mitatu ya kushindwa na adui zako, ukipatwa na upanga wao, au siku tatu za upanga wa BWANA, yaani, siku tatu za tauni katika nchi na malaika wa BWANA akiangamiza kila mahali katika Israeli.’ Sasa basi, amua jinsi nitakavyomjibu yeye aliyenituma.” Daudi akamwambia Gadi, “Ninayo mahangaiko makubwa. Mimi na nianguke mikononi mwa BWANA kwa maana rehema zake ni kuu mno, lakini usiniache niangukie mikononi mwa wanadamu.” Basi BWANA akatuma tauni katika Israeli, watu 70,000 wa Israeli wakafa. Mungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, BWANA akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa BWANA alikuwa amesimama katika sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi. Daudi akayainua macho yake akamwona huyo malaika wa BWANA akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyoosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa nguo za gunia, wakaanguka kifudifudi. Daudi akamwambia Mungu, “Je, si mimi ndiye niliyeamuru watu wahesabiwe? Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Ee BWANA, Mungu wangu, mkono wako na uwe juu yangu mimi na jamaa yangu, lakini usiache tauni hii iendelee juu ya watu wako.” Kisha malaika wa BWANA akamwamuru Gadi amwambie Daudi apande na kumjengea BWANA madhabahu kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi. Kwa hiyo Daudi akakwea, akalitii lile neno ambalo Gadi alikuwa amelisema katika jina la BWANA. Arauna alipokuwa akipura ngano, akageuka akamwona yule malaika. Wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha, yeye akaendelea kupura ngano. Kisha Daudi akakaribia, Arauna alipotazama na kumwona, akaondoka kwenye uwanja wa kupuria nafaka akamsujudia Daudi akiuinamisha uso wake ardhini. Daudi akamwambia, “Nipatie huu uwanja wako wa kupuria nafaka ili niweze kujenga madhabahu ya BWANA tauni ipate kukomeshwa katika watu. Niuzie kwa bei yake kamili.” Arauna akamwambia Daudi, “Uchukue huo uwanja. Mfalme bwana wangu na afanye lolote analopenda. Tazama, nitatoa maksai kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, vifaa vya kupuria kuwa kuni, pamoja na ngano kwa ajili ya dhabihu ya nafaka. Natoa hivi vyote.” Lakini Mfalme Daudi akamjibu Arauna, “La hasha! Lakini ninasisitiza kwamba nitalipa bei yake kamili. Sitachukua kilicho chako kwa ajili ya BWANA au kutoa sadaka ya kuteketezwa ambayo hainigharimu chochote.” Basi Daudi akamlipa Arauna shekeli za dhahabu 600 kwa ajili ya ule uwanja. Kisha Daudi akamjengea BWANA madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwita BWANA naye BWANA akajibu maombi yake kwa moto toka mbinguni juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Kisha BWANA akanena na yule malaika, naye akarudisha upanga wake katika ala yake. Wakati huo, Daudi alipoona kwamba BWANA amemjibu kule kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna Myebusi, akatoa dhabihu huko. Maskani ya BWANA ambayo Mose aliitengeneza kule jangwani, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa wakati huo vilikuwa viko mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. Lakini Daudi hakuthubutu kuisogelea ili kumuuliza Mungu, kwa sababu aliuogopa upanga wa yule malaika wa BWANA.

1 Mambo ya Nyakati 21:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Shetani akajitokeza kuwataabisha Waisraeli, akamshawishi Daudii awahesabu watu. Hivyo, Daudi akamwambia Yoabu na wale makamanda wengine, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli, kutoka Beer-sheba mpaka Dani. Nileteeni ripoti ili nijue idadi yao.” Lakini Yoabu akasema, “Mwenyezi-Mungu na awaongeze Waisraeli mara mia kuliko walivyo sasa! Bwana wangu mfalme, kwani hawa wote si watumishi wako? Kwa nini basi unataka kufanya jambo ambalo litawatia Waisraeli katika hatia?” Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu. Hivyo, Yoabu akaenda katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu. Yoabu akampelekea mfalme Daudi idadi ya watu: Katika Israeli yote, kulikuwamo wanaume 1,100,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga; na katika Yuda kulikuwamo watu 470,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga. Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. Mungu hakupendezwa na jambo hilo kwa hiyo akaiadhibu Israeli. Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo hili nililolifanya! Lakini nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.” Basi, Mwenyezi-Mungu alisema na Gadi, mwonaji wa Daudi, akamwambia, “Nenda umwambie Daudi kwamba mimi Mwenyezi-Mungu ninampa mambo matatu. Ajichagulie mojawapo nami nitamtendea.” Hivyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Jichagulie mojawapo: Njaa ya miaka mitatu, au miezi mitatu ya maangamizi kutokana na maadui zako ambapo upanga wa maadui zako utakushinda; au siku tatu ambapo Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa upanga wake, awaletee maradhi mabaya nchini, na malaika wake apite kuwaangamiza katika nchi nzima ya Israeli. Sasa amua, ni jibu lipi nitakalompa yeye aliyenituma.” Daudi akamjibu Gadi, “Nimeingia katika mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu kwani yeye ana huruma sana. Ila nisianguke katika mkono wa mwanadamu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi mabaya, ambayo yalisababisha vifo vya Waisraeli 70,000. Halafu Mungu akatuma malaika aende kuuharibu Yerusalemu; lakini kabla hajafanya hivyo, Mwenyezi-Mungu akageuza nia yake na kumwambia malaika huyo aliyetekeleza maangamizi, “Basi, yatosha!” Malaika alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Ornani, Myebusi. Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama kati ya mbingu na dunia, naye ameunyosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuuangamiza. Hapo Daudi na wazee wote walikuwa wamevaa mavazi ya gunia, wakaanguka kifudifudi. Daudi alimwambia Mungu, “Je, si mimi niliyetoa amri watu wahesabiwe? Ni mimi niliyetenda dhambi na kufanya uovu. Lakini kondoo hawa wamefanya nini? Nakusihi sana, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mkono wako uwe dhidi yangu na dhidi ya jamaa ya baba yangu, lakini maradhi haya mabaya yasiwapate watu wako.” Ndipo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwamuru Gadi amwambie Daudi aende amjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu, katika kiwanja cha kupuria nafaka cha Ornani Myebusi. Daudi akatii amri ya Mwenyezi-Mungu, akapanda juu kufuatana na neno la Gadi alilosema kwa jina la Mwenyezi-Mungu. Ornani alipogeuka na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Ornani alikuwa akipura ngano. Daudi alipomwendea Ornani, Ornani alitazama na kumwona Daudi; basi huyo Ornani alitoka kwenye uwanja wa kupuria akaenda mbele; kisha akamsujudia akiinamisha kichwa chake mpaka chini ardhini. Daudi akamwambia Ornani, “Nipe nafasi ya uwanja wako wa kupuria nafaka ili nimjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu juu yake, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa kwa watu. Niuzie kwa bei yake kamili.” Naye Ornani akamwambia Daudi, “Kichukue kiwanja hiki, bwana wangu mfalme, na ukitumie vile unavyopenda mwenyewe. Tazama, nawatoa fahali kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, na vifaa vya kupuria kwa kuni, pamoja na ngano iwe tambiko ya nafaka. Vyote hivyo ninakupa.” Lakini mfalme Daudi alimwambia Ornani, “La, hasha; nitavinunua kwa thamani yake kamili; sitamchukulia Mwenyezi-Mungu kitu kilicho chako au kumtolea tambiko za kuteketezwa ambazo hazijanigharimu kitu.” Hivyo, Daudi alimlipa Ornani kwa kumpimia shekeli 600 kamili za dhahabu kulipia uwanja huo. Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu mahali hapo na kumtolea sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akakubali ombi lake kwa kuleta moto kutoka mbinguni kuiteketeza ile sadaka kwenye madhabahu. Halafu, Mwenyezi-Mungu alimwamuru malaika, naye akaweka upanga wake alani mwake. Wakati huo, Daudi alipoona ya kwamba Mwenyezi-Mungu amekubali ombi lake kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Ornani, Myebusi, akatoa tambiko papo hapo. Hema la Mwenyezi-Mungu ambalo lilitengenezwa na Mose nyikani, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, wakati huo vilikuwa bado pale mahali pa kuabudia huko Gibeoni. Lakini Daudi hakuweza kwenda huko kumwomba Mungu shauri kwa sababu alikuwa anauogopa upanga wa malaika wa Mwenyezi-Mungu.

1 Mambo ya Nyakati 21:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Waisraeli. Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao. Naye Yoabu akasema, BWANA na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona alete hatia kwa Israeli? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu. Naye Yoabu akamtolea Daudi jumla ya hesabu ya watu. Na hao wote wa Israeli walikuwa watu milioni moja na laki moja, wenye kufuta panga; na wa Yuda watu elfu mia nne sabini (470,000), wenye kufuta panga. Lakini Lawi na Benyamini hakuwahesabu miongoni mwao; kwa sababu neno la mfalme limemchukiza Yoabu. Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli. Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. Naye BWANA akanena na Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema, Nenda ukanene na Daudi, ukisema, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, BWANA asema hivi, Jichagulie upendavyo; miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa BWANA, yaani tauni katika nchi, na malaika wa BWANA akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. Basi BWANA akawaletea Israeli tauni; nao wakaanguka wa Israeli watu elfu sabini. Naye Mungu akatuma malaika aende Yerusalemu ili auangamize; naye alipokuwa tayari kuangamiza, BWANA akatazama, akaghairi katika mabaya, akamwambia malaika aharibuye, Basi yatosha; sasa ulegeze mkono wako. Naye malaika wa BWANA akasimama karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa BWANA amesimama kati ya nchi na mbingu, naye alikuwa na upanga wazi mkononi, umenyoshwa juu ya Yerusalemu. Ndipo Daudi na wazee wakaanguka kifudifudi, nao wamevaa nguo za magunia. Daudi akamwambia Mungu, Je! Si mimi niliyeamuru watu wahesabiwe? Naam, mimi ndimi niliyekosa, na kufanya yaliyo maovu sana; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako, nakusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya babangu; wala si juu ya watu wako, hata wao wapigwe. Ndipo huyo malaika wa BWANA akamwamuru Gadi kwamba amwambie Daudi, ya kuwa Daudi akwee, akamwinulie BWANA madhabahu katika kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea kulingana na neno la Gadi, alilolinena kwa jina la BWANA. Arauna alipogeuka, na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Arauna alikuwa akipura ngano. Basi Daudi alipokuwa akimjia Arauna, Arauna akatazama, akamwona Daudi, akatoka katika kile kiwanja, akamsujudia Daudi kifudifudi hadi chini. Ndipo Daudi akamwambia Arauna, Unipe mahali pa kiwanja hiki, ili kwamba nimjengee BWANA madhabahu hapa; kwa thamani yake kamili utanipa; ili kwamba tauni izuiliwe katika watu. Arauna akamwambia Daudi, Ujitwalie, na bwana wangu mfalme na afanye yaliyo mema machoni pake; tazama, ng'ombe kwa sadaka za kuteketezwa, na vyombo vya kupuria kwa kuni, na ngano kwa sadaka ya unga, nazitoa; zote nazitoa. Mfalme Daudi akamwambia Arauna, La, sivyo, lakini kweli nitazinunua kwa thamani yake kamili; kwani sitamtwalia BWANA kilicho chako, wala kutoa sadaka ya kuteketezwa isiyo na gharama. Basi Daudi akampimia Arauna thamani ya mahali pale shekeli mia sita za dhahabu kwa uzani Kisha Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, akamlingana BWANA; naye akamwitikia kutoka mbinguni kwa moto juu ya madhabahu hiyo ya sadaka ya kuteketezwa. BWANA naye akamwamuru malaika; naye akaurudisha upanga wake alani mwake tena. Wakati huo, Daudi alipoona ya kwamba BWANA amemwitikia katika kiwanja cha Arauna, Myebusi, ndipo alipotoa dhabihu huko. Kwa maana ile maskani ya BWANA, aliyoifanya Musa jangwani, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, vilikuwapo wakati huo mahali pa juu pa Gibeoni. Wala Daudi hakuweza kwenda mbele yake ili kumwuliza Mungu; kwa sababu aliona hofu kwa ajili ya upanga wa yule malaika wa BWANA.

1 Mambo ya Nyakati 21:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli. Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao. Naye Yoabu akasema, BWANA na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona awe sababu ya hatia kwa Israeli? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu. Naye Yoabu akamtolea Daudi jumla ya hesabu ya watu. Na hao wote wa Israeli walikuwa watu elfu mara elfu, na mia elfu, wenye kufuta panga; na wa Yuda watu mia nne na sabini elfu, wenye kufuta panga. Lakini Lawi na Benyamini hakuwahesabu miongoni mwao; kwa sababu neno la mfalme limemchukiza Yoabu. Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli. Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumwa wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. Naye BWANA akanena na Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema, Nenda ukanene na Daudi, ukisema, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, BWANA asema hivi, Kubali upendavyo; miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa BWANA, yaani tauni katika nchi, na malaika wa BWANA akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. Basi BWANA akawaletea Israeli tauni; nao wakaanguka wa Israeli watu sabini elfu. Naye Mungu akatuma malaika aende Yerusalemu ili auangamize; naye alipokuwa tayari kuangamiza, BWANA akatazama, akaghairi katika mabaya, akamwambia malaika aharibuye, Basi yatosha; sasa ulegeze mkono wako. Naye malaika wa BWANA akasimama karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa BWANA amesimama kati ya nchi na mbingu, naye alikuwa na upanga wazi mkononi, umenyoshwa juu ya Yerusakmu. Ndipo Daudi na wazee wakaanguka kifulifuli, nao wamevaa nguo za magunia. Daudi akamwambia Mungu, Je! Si mimi niliyeamuru watu wahesabiwe? Naam, mimi ndimi niliyekosa, na kufanya yaliyo maovu sana; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako, nakusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya babangu; wala si juu ya watu wako, hata wao wapigwe. Ndipo huyo malaika wa BWANA akamwamuru Gadi kwamba amwambie Daudi, ya kuwa Daudi akwee, akamwinulie BWANA madhabahu katika kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi. Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, alilolinena kwa jina la BWANA. Arauna alipogeuka, na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Arauna alikuwa akipura ngano. Basi Daudi alipokuwa akimjia Arauna, Arauna akatazama, akamwona Daudi, akatoka katika kile kiwanja, akamsujudia Daudi kifulifuli hata nchi. Ndipo Daudi akamwambia Arauna, Unipe mahali pa kiwanja hiki, ili kwamba nimjengee BWANA madhabahu hapa; kwa thamani yake kamili utanipa; ili kwamba tauni izuiliwe katika watu. Arauna akamwambia Daudi, Ujitwalie, na bwana wangu mfalme na afanye yaliyo mema machoni pake; tazama, ng’ombe kwa sadaka za kuteketezwa, na vyombo vya kupuria kwa kuni, na ngano kwa sadaka ya unga, nazitoa; zote nazitoa. Mfalme Daudi akamwambia Arauna, La, sivyo, lakini kweli nitazinunua kwa thamani yake kamili; kwani sitamtwalia BWANA kilicho chako, wala kutoa sadaka ya kuteketezwa isiyo na gharama. Basi Daudi akampimia Arauna thamani ya mahali pale shekeli mia sita za dhahabu kwa uzani Kisha Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, akamlingana BWANA; naye akamwitikia kutoka mbinguni kwa moto juu ya madhabahu hiyo ya sadaka ya kuteketezwa. BWANA naye akamwamuru malaika; naye akaurudisha upanga wake alani mwake tena. Wakati huo, Daudi alipoona ya kwamba BWANA amemwitikia katika kiwanja cha Arauna, Myebusi, ndipo hutoa dhabihu huko. Kwa maana ile maskani ya BWANA, aliyoifanya Musa jangwani, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, vilikuwapo wakati huo mahali pa juu pa Gibeoni. Wala Daudi hakuweza kwenda mbele yake ili kumwuliza Mungu; kwa sababu aliona hofu kwa ajili ya upanga wa yule malaika wa BWANA.