Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 19:1-19

1 Mambo ya Nyakati 19:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa baada ya hayo, Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, akafa, akamiliki mwanawe mahali pake. Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi, kwa kuwa babaye alinitendea mimi wema. Basi Daudi akapeleka wajumbe ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni kwa Hanuni, ili wamtulize. Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, Je! Waona Daudi amheshimu babayo kwa kukupelekea wafariji? Je! Hawakukujia watumishi wake ili kuiangalia nchi, na kuiangamiza, na kuipeleleza? Basi Hanuni akawatwaa watumishi wa Daudi, akawanyoa, akawakatia nguo zao katikati, hata matakoni, akawatoa waende zao. Wakaenda watu wakamwambia Daudi jinsi walivyotendewa wale watu. Naye akatuma watu kuwalaki; kwa sababu watu hao walikuwa wametahayarika sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hata mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi. Na wana wa Amoni walipoona ya kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, Hanuni na wana wa Amoni wakapeleka talanta elfu za fedha ili kujiajiria magari na wapanda farasi kutoka Mesopotamia, na kutoka Atam-maaka, na kutoka Soba. Basi wakajiajiria magari thelathini na mbili elfu, na mfalme wa Maaka na watu wake; nao walikuja wakatua mbele ya Medeba. Na wana wa Amoni wakakusanyika kutoka miji yao, wakaja vitani. Basi Daudi aliposikia habari akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa. Wakatoka wana wa Amoni, wakapanga vita langoni pa mji; na hao wafalme waliokuja walikuwa peke yao uwandani. Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami. Na hao watu waliosalia akawatia mikononi mwa Abishai, nduguye, nao wakajipanga juu ya wana wa Amoni. Akasema, Wakiwa Washami ni hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia; lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakusaidia wewe. Uwe hodari, tukajitie moyo mkuu kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye BWANA afanye yaliyo mema machoni pake. Basi Yoabu, na watu waliokuwa pamoja naye, wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake. Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, nduguye, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akaja Yerusalemu. Na Washami walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, wakapeleka wajumbe, wakawavuta Washami walioko ng’ambo ya Mto, na Shobaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri, akawaongoza. Alipoambiwa Daudi; akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akawajia, akapanga vita juu yao. Basi Daudi alipopanga vita juu ya Washami, wakapigana naye. Washami wakakimbia mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami watu wa magari saba elfu, na askari waendao kwa miguu arobaini elfu, akamwua na Shobaki, jemadari wa jeshi. Na watumwa wa Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Daudi, wakamtumikia; wala Washami hawakukubali kuwasaidia wana wa Amoni tena.

1 Mambo ya Nyakati 19:1-19 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya muda, Nahashi mfalme wa Waamoni akafa, mwanawe akaingia mahali pake. Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kwa sababu baba yake alinitendea wema.” Hivyo Daudi akatuma wajumbe ili kumfariji Hanuni kwa ajili ya kifo cha baba yake. Watu wa Daudi walipofika kwa Hanuni katika nchi ya Waamoni ili kumfariji, wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni, “Hivi unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kuwatuma wajumbe kukufariji? Je, hawa watu hawakuja kuipeleleza na kuidadisi nchi ili waishinde?” Kwa hiyo Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa ndevu akakata nguo zao katikati kwenye matako, akawaacha waende zao. Mtu mmoja alipofika na kumpasha Daudi habari za watu hawa, akawatuma wajumbe wengine kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko mpaka ndevu zenu ziote, ndipo mje.” Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, Hanuni na Waamoni wakatuma talanta 1,000 za fedha ili kukodisha magari ya vita pamoja na waendeshaji wa hayo magari ya kukokotwa na farasi, kutoka Aramu-Naharaimu, Aramu-Maaka na Soba. Wakakodisha magari ya vita 32,000 yakiwa na waendeshaji wake, pamoja na mfalme wa Maaka na vikosi vyake, wakaja na kupiga kambi karibu na Medeba. Waamoni nao wakakusanyika toka miji yao, wakatoka ili kupigana vita. Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji. Waamoni wakatoka wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati wale wafalme wengine waliokuja nao walijipanga kwa vita uwanjani. Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu. Akawaweka wale wanajeshi wengine waliobaki chini ya amri ya Abishai ndugu yake, nao wakapangwa ili wakabiliane na Waamoni. Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itakupasa wewe unisaidie; lakini kama Waamoni watakuzidi nguvu, basi mimi nitakusaidia. Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. BWANA atafanya lile lililo jema machoni pake.” Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake. Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao pia wakakimbia mbele ya nduguye Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi Yerusalemu. Baada ya Waaramu kuona kwamba wameshindwa na Israeli, wakapeleka wajumbe na kuwataka Waaramu wengine kutoka ngʼambo ya Mto Frati, wakiongozwa na Shofaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri. Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote na kuvuka Yordani. Akasonga mbele dhidi yao na akajipanga kuwakabili. Daudi akapanga vita ili kupigana na Waaramu, nao wakapigana dhidi yake. Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari 7,000 na askari wao wa miguu 40,000. Pia akamuua Shofaki, jemadari wa jeshi lao. Raiya wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya mapatano ya amani na Daudi, wakawa watumishi wake. Hivyo Waaramu hawakukubali kuwasaidia Waamoni tena.

1 Mambo ya Nyakati 19:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Ikawa baada ya hayo Nahashi, mfalme wa Waamoni akafariki; naye mwanawe akashika utawala. Basi, Daudi akasema, “Nitamtendea mema Hanuni mwana wa Nahashi, kwani baba yake alinitendea mema pia.” Hivyo Daudi alituma wajumbe na kumpelekea salamu za rambirambi kwa ajili ya kifo cha baba yake. Nao wakaenda kwa Hanuni ili kumfariji, huko katika nchi ya Waamoni. Lakini viongozi wa Waamoni wakamwambia mfalme, “Je! Unadhani ni kwa sababu ya heshima ya baba yako ati Daudi ametuma wajumbe hawa waje kukufariji? Watu hawa si majasusi waliotumwa kuja kuichunguza nchi kuiangamiza na kuipeleleza?” Basi Hanuni aliwachukua wajumbe hao wa Daudi, akawanyoa ndevu na kuzipasua nguo zao katikati hadi matakoni, kisha akawatoa waende zao, nao wakaondoka kurudi makwao. Daudi alipopashwa habari jinsi walivyotendewa wajumbe wake, alituma watu kuwalaki kwani hao wajumbe waliona aibu sana. Naye mfalme aliwaambia, “Kaeni mjini Yeriko, hata mtakapoota ndevu, Kisha mrudi.” Waamoni walipoona wamejifanya wachukizwe na Daudi, Hanuni na hao Waamoni walituma watu wapeleke talanta 4,000 za fedha kukodisha magari na wapandafarasi kutoka Mesopotamia, Aramaaka na Soba. Walikodisha magari 32,000 na mfalme wa Maaka na askari wake, akaja na kupiga kambi karibu na Medeba. Waamoni walikusanyika toka kwenye miji yao yote, wakajiandaa tayari kwa vita. Naye Daudi aliposikia habari hizo alimtuma Yoabu na jeshi lote la mashujaa. Waamoni walitoka wakajipanga kwenye lango la mji, hali wale wafalme waliokuja walikuwa peke yao kwenye tambarare. Yoabu alipoona kuwa vita ni vikali dhidi yake, mbele na nyuma, aliwateua baadhi ya wanajeshi hodari zaidi wa Waisraeli, akawapanga kukabiliana na Waaramu. Wale wanajeshi wengine waliobaki, aliwaweka chini ya uongozi wa Abishai ndugu yake, naye akawapanga ili wakabiliane na Waamoni. Yoabu akamwambia Abishai, “Ikiwa Waaramu wananizidi nguvu, utanisaidia; lakini kama Waamoni wanakuzidi nguvu, nitakuja kukusaidia. Basi jipe moyo! Tupigane kiume kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; na Mwenyezi-Mungu atutendee lile analoona ni jema kwake.” Basi, Yoabu na watu wake walisonga mbele kupigana na Wasiria; nao Waaramu walikimbia. Waamoni walipoona Waaramu wamekimbia, nao walimkimbia Abishai, nduguye Yoabu, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akarudi Yerusalemu. Lakini Waaramu walipoona ya kwamba wameshindwa na Waisraeli, walituma wajumbe waende kuwaleta Waaramu wengine waliokuwa ngambo ya mto Eufrate wakiongozwa na Shofaki, kamanda wa jeshi la Hadadezeri. Daudi alipopata habari, aliwakusanya pamoja Waisraeli wote, akavuka mto Yordani, akawaendea, akapanga vikosi vyake dhidi yao. Daudi alipopanga vita dhidi ya Wasiria, basi nao walipigana naye. Lakini Waaramu walikimbia mbele ya Waisraeli. Daudi aliwaua Waaramu waendeshao magari 7,000 na askari wa miguu 40,000. Pia alimuua Shofaki, kamanda wa jeshi lao. Kisha watumishi wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Waisraeli, walifanya mapatano ya amani na Daudi nao wakawa watumishi wa Daudi. Hivyo Waaramu hawakukubali kuwasaidia Waamoni tena.

1 Mambo ya Nyakati 19:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa baada ya hayo, Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, akafa, akatawala mwanawe mahali pake. Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi, kwa kuwa babaye alinitendea mimi wema. Basi Daudi akatuma wajumbe ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni kwa Hanuni, ili wamtulize. Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, Je! Unadhani Daudi amewatuma wafariji kwako kwa heshima ya baba yako? Je! Hawakukujia watumishi wake ili kuichunguza nchi, na kuiangamiza, na kuipeleleza? Basi Hanuni akawatwaa watumishi wa Daudi, akawanyoa, akawapasulia nguo zao katikati, hadi kiunoni, kisha akawaachilia waondoke. Ndipo wakaondoka. Watu walipomwambia Daudi jinsi wajumbe wake walivyotendewa, alituma watu kuwalaki; kwa sababu walikuwa wameaibishwa sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hadi mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi. Na wana wa Amoni walipoona ya kuwa wamejisababishia machukizo kwa Daudi, Hanuni na wana wa Amoni wakatuma talanta elfu moja za fedha ili kukodi magari na wapanda farasi kutoka Mesopotamia, na kutoka Atam-maaka, na kutoka Soba. Basi wakakodi magari elfu thelathini na mbili, na mfalme wa Maaka na watu wake; nao walikuja wakatua mbele ya Medeba. Na wana wa Amoni wakakusanyika kutoka miji yao, wakaja vitani. Basi Daudi aliposikia habari akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa. Wakatoka wana wa Amoni, wakajipanga kwa vita langoni pa mji; na hao wafalme waliokuja walikuwa peke yao uwanjani. Basi Yoabu alipoona ya kwamba wamejipanga kwa vita juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami. Na hao watu waliosalia akawatia mikononi mwa Abishai, nduguye, nao wakajipanga juu ya wana wa Amoni. Akasema, Washami wakiwa ni hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia; lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakusaidia wewe. Kuwa hodari, tuwe na ujasiri, kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye BWANA afanye yaliyo mema machoni pake. Basi Yoabu, na watu waliokuwa pamoja naye, wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake. Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, nduguye, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akaja Yerusalemu. Na Washami walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, wakatuma wajumbe, wakawaleta Washami walioko ng'ambo ya Mto, na Shobaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri, akawaongoza. Alipoambiwa Daudi; akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akawajia, akapanga vita juu yao. Basi Daudi alipopanga vita juu ya Washami, wakapigana naye. Washami wakakimbia mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami watu wa magari elfu saba, na askari waendao kwa miguu elfu arubaini, akamwua na Shobaki, jemadari wa jeshi. Na watumishi wa Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Daudi, wakamtumikia; wala Washami hawakukubali kuwasaidia wana wa Amoni tena.