1 Mambo ya Nyakati 17:11-14
1 Mambo ya Nyakati 17:11-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku zako zitakapotimia za kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako, wewe mwenyewe awe mfalme; nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba; nami nitahakikisha kwamba ufalme wake unadumu milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; lakini sitamwondolea fadhili zangu kama vile nilivyomwondolea Shauli aliyekutangulia. Bali nitamwimarisha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele, na kiti chake cha enzi kitakuwa imara daima.’”
1 Mambo ya Nyakati 17:11-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende kulala pamoja na baba zako, nitainua mzawa wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakiimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako; ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele.
1 Mambo ya Nyakati 17:11-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende na babazo, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wake milele. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako; ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele.
1 Mambo ya Nyakati 17:11-14 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Wakati wako utakapokuwa umekwisha, nawe ukawa umekwenda kukaa na baba zako, nitamwinua mzao wako aingie mahali pako kuwa mfalme, mmoja wa wana wako mwenyewe, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili yangu, nami nitakifanya imara kiti cha ufalme wake milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Kamwe sitaondoa upendo wangu kwake, kama nilivyouondoa kwa yeye aliyekutangulia. Nitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele; kiti chake cha enzi nitakifanya imara milele.’ ”