Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 17:1-15

1 Mambo ya Nyakati 17:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Baada ya Daudi kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mierezi, wakati Sanduku la Agano la BWANA liko ndani ya hema.” Nathani akamjibu Daudi, “Lolote ulilo nalo moyoni mwako litende, kwa maana Mungu yu pamoja nawe.” Usiku ule neno la Mungu likamjia Nathani, kusema: “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Wewe hutanijengea mimi nyumba ili nikae humo. Mimi sijakaa ndani ya nyumba tangu siku ile niliyowatoa Israeli kutoka Misri mpaka leo. Nimehama kutoka hema moja hadi jingine na kutoka mahali pamoja hadi pengine. Je, popote nilipokwenda pamoja na Waisraeli wote, wakati wowote nilimwambia kiongozi yeyote niliyemwagiza kuwachunga watu wangu, kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?’  “Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: Nilikuchukua machungani na kutoka kuandama kondoo ili uwatawale watu wangu Israeli. Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani. Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali na nitawapa ili wawe na mahali pao wenyewe pa kuishi na wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni, na ambavyo wamefanya siku zote tangu nilipowachagua viongozi kwa ajili ya watu wangu Israeli. Pia nitawatiisha adui zenu wote. “ ‘Pamoja na hayo ninakuambia kwamba BWANA atakujengea nyumba: Wakati wako utakapokuwa umekwisha, nawe ukawa umekwenda kukaa na baba zako, nitamwinua mzao wako aingie mahali pako kuwa mfalme, mmoja wa wana wako mwenyewe, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili yangu, nami nitakifanya imara kiti cha ufalme wake milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Kamwe sitaondoa upendo wangu kwake, kama nilivyouondoa kwa yeye aliyekutangulia. Nitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele; kiti chake cha enzi nitakifanya imara milele.’ ” Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.

1 Mambo ya Nyakati 17:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, siku moja alimwita nabii Nathani, na kumwambia, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mwerezi, lakini sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu linakaa hemani.” Nathani akamwambia Daudi, “Fanya chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.” Lakini usiku uleule, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani, kusema, “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa. Tangu wakati ule nilipowaongoza watu wa Israeli kutoka Misri mpaka hivi leo, sijaishi kwenye nyumba. Nimekuwa nikihama toka hema hadi hema, na toka makao hadi makao mengine. Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli, nimepata kumwuliza mwamuzi wao yeyote niliyemwamuru awachunge watu wangu, “Kwa nini hukunijengea nyumba ya mierezi?” ’ Kwa hiyo basi, mwambie mtumishi wangu Daudi: ‘Mwenyezi-Mungu wa majeshi anasema hivi: Nilikutoa malishoni ulipokuwa unawachunga kondoo, ili uwe mkuu wa watu wangu Israeli. Tangu wakati huo nimekuwa pamoja nawe kokote ulikokwenda na nimewaangamiza maadui zako wote mbele yako. Nitakufanya kuwa maarufu kama wakuu wengine wa dunia. Nami nitawachagulia watu wangu wa Israeli mahali pa kuishi niwapandikize, ili waishi mahali pao wenyewe, wasisumbuliwe tena. Nao watu wakatili wanaotumia nguvu hawatawatesa tena kama hapo awali, tangu wakati nilipowateua waamuzi juu ya watu wangu Israeli; mimi nitawashinda maadui zako wote. Zaidi ya yote, mimi Mwenyezi-Mungu nakutangazia kuwa nitakujengea nyumba. Siku zako zitakapotimia za kujiunga na babu zako, nitamfanya mmoja wa watoto wako, wewe mwenyewe awe mfalme; nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba; nami nitahakikisha kwamba ufalme wake unadumu milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; lakini sitamwondolea fadhili zangu kama vile nilivyomwondolea Shauli aliyekutangulia. Bali nitamwimarisha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele, na kiti chake cha enzi kitakuwa imara daima.’” Nathani alimwelezea Daudi mambo yote haya kulingana na maono yote.

1 Mambo ya Nyakati 17:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, Daudi alipokuwa akikaa nyumbani mwake, Daudi akamwambia nabii Nathani, Angalia, mimi ninakaa katika nyumba ya mwerezi, bali sanduku la Agano la BWANA linakaa chini ya mapazia. Naye Nathani akamwambia Daudi, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; kwa maana Mungu yu pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la Mungu likamjia Nathani, kusema, Nenda, kamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa; kwa maana sikukaa ndani ya nyumba tangu siku ile nilipowaleta Israeli huku hata leo; lakini hema kwa hema nimehamia, na maskani kwa maskani. Katika mahali kote nilikokwenda na Israeli wote, je! Nimesema neno lolote na mtu yeyote wa waamuzi wa Israeli, niliowaagiza kuwalisha watu wangu, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mwerezi? Basi sasa ndivyo utakavyomwambia mtumishi wangu Daudi, BWANA wa majeshi asema hivi, Nilikutwaa kutoka machungani, hata katika kuwafuata kondoo ili uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina, kama jina la hao wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia watu wangu Israeli mahali, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena kama hapo kwanza, na tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi wawatawale watu wangu Israeli, nami nitawashinda adui zako wote. Pamoja na hayo nakuambia, ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende kulala pamoja na baba zako, nitainua mzawa wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitauimarisha ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakiimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako; ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele. Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.

1 Mambo ya Nyakati 17:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, Daudi alipokuwa akikaa nyumbani mwake, Daudi akamwambia nabii Nathani, Angalia, mimi ninakaa katika nyumba ya mwerezi, bali sanduku la agano la BWANA linakaa chini ya mapazia. Naye Nathani akamwambia Daudi, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; kwa maana Mungu yu pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la Mungu likamjia Nathani, kusema, Nenda, kamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa; kwa maana sikukaa ndani ya nyumba tangu siku ile nilipowaleta Israeli huku hata leo; lakini hema kwa hema nimehamia, na maskani kwa maskani. Katika mahali mwote nilimokwenda na Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliowaagiza kuwalisha watu wangu, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mwerezi? Basi sasa ndivyo utakavyomwambia mtumishi wangu Daudi, BWANA wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo ili uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina, kama jina la hao wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia watu wangu Israeli mahali, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena kama hapo kwanza, na tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi wawe juu ya watu wangu Israeli, nami nitawashinda adui zako wote. Pamoja na hayo nakuambia, ya kwamba BWANA atakujengea nyumba. Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende na babazo, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wake milele. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako; ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele. Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.