Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 14:1-17

1 Mambo ya Nyakati 14:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha mfalme Hiramu wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi, pia alimpelekea mierezi, waashi na maseremala, ili wamjengee Daudi ikulu. Hivyo, Daudi akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu amemwimarisha awe mfalme wa Israeli, na kwamba ufalme wake umekuzwa kwa ajili ya Israeli, watu wake. Huko Yerusalemu, Daudi alioa wake wengi zaidi, naye akazaa wana na mabinti wengine. Yafuatayo ndio majina ya watoto aliozaa huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, Ibhari, Elishua, Elpeleti, Noga, Nefegi, Yafia, Elishama, Beeliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa nchi nzima ya Israeli, wote walitoka kwa wingi kwenda kumtafuta. Daudi alipopata habari, alitoka kwenda kuwakabili. Wafilisti walifika wakaanza mashambulizi katika bonde la Refaimu. Ndipo Daudi alipomwuliza Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.” Basi, Daudi akaenda huko Baal-perasimu, akawashinda; halafu akasema, “Mungu amepita katikati ya adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji yaendayo kasi.” Kwa hiyo mahali hapo panaitwa Baal-perasimu. Wafilisti walipokimbia, waliziacha sanamu za miungu yao huko, naye Daudi akatoa amri zote zichomwe moto. Kisha Wafilisti walifanya mashambulizi katika bonde hilo kwa mara ya pili. Safari hii, Daudi alipoomba shauri kwa Mungu, Mungu akamwambia, “Usiwashambulie kutoka hapa, ila zunguka na kuwashambulia kutoka mkabala na miti ya miforosadi, halafu washambulie kutoka huko. Na mara utakaposikia vishindo vya gwaride kwenye vilele vya hiyo miforosadi, haya, toka uende vitani. Nitakuwa nimekwisha kukutangulia kulipiga jeshi la Wafilisti.” Daudi alifanya kama alivyoamriwa na Mungu. Alilipiga jeshi la Wafilisti kutoka Gibeoni hadi Gezeri. Daudi akawa maarufu kote nchini, naye Mwenyezi-Mungu akayatia hofu mataifa yote, nayo yakamwogopa sana.

1 Mambo ya Nyakati 14:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na waashi, na maseremala, ili wamjengee nyumba. Daudi akajua ya kwamba BWANA amemweka imara ili atawale Israeli, na kwamba milki yake imetukuka zaidi kwa ajili ya watu wake Israeli. Tena Daudi akazidi kuoa wake huko Yerusalemu; akazidi kuzaa wana na binti. Na haya ndiyo majina ya watoto aliozaliwa huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani; na Ibhari, na Elishua, na Elpeleti; na Noga, na Nefegi, na Yafia; na Elishama, na Eliada, na Elifeleti. Wafilisti waliposikia ya kwamba Daudi ametiwa mafuta ili awe mfalme wa Israeli wote, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akasikia, akatoka nje kupigana nao. Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya katika bonde la Warefai. Daudi akamwuliza Mungu, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye BWANA akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako. Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, BWANA amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu. Nao wakaiacha miungu yao huko; naye Daudi akaamuru, ikateketezwa kwa moto. Lakini hao Wafilisti wakajitawanya tena mara ya pili bondeni. Na Daudi akamwuliza Mungu tena; naye Mungu akamwambia, Hutapanda kuwafuata; zunguka mbali nao, na kuwajia ukielekea miforsadi. Kisha itakuwa utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo utakapokwenda nje vitani; kwa maana ndipo Mungu ametoka mbele yako, awapige jeshi la Wafilisti. Daudi akafanya kama vile Mungu alivyomwamuru; wakawapiga jeshi la Wafilisti toka Geba mpaka Gezeri. Sifa za Daudi zikafika nchi zote; naye BWANA akawaletea mataifa yote hofu yake.

1 Mambo ya Nyakati 14:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Naye Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na waashi, na maseremala, ili wamjengee nyumba. Daudi akajua ya kwamba BWANA amemweka imara ili amiliki juu ya Israeli, kwa kuwa milki yake imeinuka kwa ajili ya watu wake Israeli. Tena Daudi akazidi kuoa wake huko Yerusalemu; akazidi Daudi kuzaa wana na binti. Na haya ndiyo majina ya watoto aliozaliwa huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani; na Ibhari, na Elishua, na Elpeleti; na Noga, na Nefegi, na Yafia; na Elishama, na Eliada, na Elifeleti. Na waliposikia hao Wafilisti ya kwamba Daudi ametiwa mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli wote, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akasikia, akatoka nje kupigana nao. Basi hao Wafilisti walikuwa wamekuja na kuteka nyara katika bonde la Warefai. Daudi akamwuliza Mungu, kusema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye BWANA akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako. Basi wakapanda mpaka Baal-perasimu, Daudi naye akawapiga huko; Daudi akasema, BWANA amewafurikia adui zangu kwa mkono wangu, kama mafuriko ya maji. Basi wakapaita mahali pale jina lake Baal-perasimu. Nao wakaiacha miungu yao huko; naye Daudi akaamuru, ikateketezwa kwa moto. Lakini hao Wafilisti wakateka nyara tena mara ya pili bondeni. Na Daudi akamwuliza Mungu tena; naye Mungu akamwambia, Hutapanda kuwafuata; uwageukie mbali, ukawajie huko kuielekea miforsadi. Kisha itakuwa utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo utakapokwenda nje vitani; kwa maana ndipo Mungu ametoka mbele yako, awapige jeshi la Wafilisti. Daudi akafanya kama vile Mungu alivyomwamuru; wakawapiga jeshi la Wafilisti toka Geba mpaka Gezeri. Sifa za Daudi zikafika nchi zote; naye BWANA akawaletea mataifa yote hofu yake.

1 Mambo ya Nyakati 14:1-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi Hiramu mfalme wa Tiro akawatuma wajumbe kwa Daudi, wakiwa na magogo ya mierezi, waashi na maseremala ili kumjengea jumba la kifalme. Naye Daudi akatambua kwamba BWANA amemwimarisha kuwa mfalme juu ya Israeli na kwamba ufalme wake umetukuzwa kwa ajili ya Israeli, watu wake. Huko Yerusalemu Daudi akaoa wake wengine zaidi na akawa baba wa wana na mabinti wengi. Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, Ibihari, Elishua, Elpeleti, Noga, Nefegi, Yafia, Elishama, Beeliada na Elifeleti. Wafilisti waliposikia kuwa Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli yote, wakapanda na jeshi lao lote kwenda kumsaka, lakini Daudi akapata habari hizo, naye akatoka ili kwenda kukabiliana nao. Basi Wafilisti walikuwa wameingia na kushambulia Bonde la Warefai, Hivyo Daudi akamuuliza Mungu: “Je, niende kuwashambulia hao Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” BWANA akamjibu, “Nenda, nitawatia mikononi mwako.” Hivyo Daudi pamoja na watu wake wakakwea mpaka Baal-Perasimu, akawashinda huko. Akasema, “Kama maji yafurikavyo, Mungu amewafurikia adui zangu kwa kutumia mkono wangu.” Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Baal-Perasimu. Wafilisti walikuwa wameacha miungu yao huko, Daudi akaamuru iteketezwe kwa moto. Kwa mara nyingine Wafilisti wakavamia lile bonde; hivyo Daudi akamuuliza Mungu tena, naye Mungu akamjibu, “Usiwapandie moja kwa moja, bali wazungukie na uwashambulie kutoka mbele ya hiyo miti ya miforosadi. Mara usikiapo sauti ya kwenda juu ya hiyo miti ya miforosadi, hapo ndipo utoke upigane vita, kwa sababu hiyo itaonyesha kwamba Mungu amekutangulia ili kupiga jeshi la Wafilisti.” Kwa hiyo Daudi akafanya kama alivyoagizwa na Mungu, wakalipiga jeshi la Wafilisti kuanzia Gibeoni hadi Gezeri. Hivyo umaarufu wa Daudi ukaenea katika kila nchi, naye BWANA akayafanya mataifa yote kumwogopa Daudi.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha