Ufunuo 21:10-27
Ufunuo 21:10-27 BHN
Basi, Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni, uking'aa kwa utukufu wa Mungu. Mwangaza wake ulikuwa kama wa jiwe la thamani kubwa kama yaspi, angavu kama kioo. Ulikuwa na ukuta mrefu na mkubwa, wenye milango kumi na miwili, na kila mmoja ulilindwa na malaika. Juu ya kila mlango paliandikwa mojawapo ya majina ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Kila upande ulikuwa na milango mitatu: Upande wa mashariki milango mitatu, kaskazini milango mitatu, kusini milango mitatu na magharibi milango mitatu. Kuta za mji huo zilikuwa zimejengwa juu ya mawe ya msingi kumi na mawili, na juu ya kila jiwe palikuwa pameandikwa mojawapo ya majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo. Basi, yule malaika aliyekuwa anasema nami alikuwa na kijiti cha dhahabu cha kupimia, kwa ajili ya kuupima huo mji, milango yake na kuta zake. Mji wenyewe ulikuwa wa mraba, upana na urefu wake sawa. Basi, malaika akaupima mji huo kwa kijiti chake: Ulikuwa na urefu, upana na kimo cha kama kilomita 2,400. Kisha akaupima ukuta wake pia; nao ulikuwa mita 60 kwa kipimo cha macho cha kibinadamu ambacho malaika alitumia. Ukuta huo ulikuwa umejengwa kwa mawe mekundu ya thamani, na mji wenyewe ulikuwa umejengwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo. Mawe ya msingi wa ukuta huo yalikuwa yamepambwa kwa kila aina ya mawe ya thamani. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa jiwe la thamani jekundu, la pili johari ya rangi ya samawati, la tatu kalkedoni, la nne zumaridi, la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolito, la nane zabarajadi, la tisa topazi, la kumi krisopraso, la kumi na moja yasintho, na la kumi na mbili amethisto. Na ile milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili; kila mlango ulikuwa umetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji ilikuwa imetengenezwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo. Sikuona hekalu katika mji huo, maana Bwana Mungu Mwenye Nguvu na yule Mwanakondoo ndio hekalu lake. Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, maana utukufu wa Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwanakondoo. Watu wa mataifa watatembea katika mwanga wake na wafalme wa dunia watauletea utajiri wao. Milango ya mji huo itakuwa wazi mchana wote; maana hakutakuwa na usiku humo. Fahari na utajiri wa watu wa mataifa utaletwa humo ndani. Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni wale tu walioandikwa katika kitabu cha uhai cha Mwanakondoo ndio watakaoingia ndani.