Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ufunuo 10:1-7

Ufunuo 10:1-7 BHN

Kisha, nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto. Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na wa kushoto juu ya nchi kavu, na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo. Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: “Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!” Kisha, yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni, akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, “Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha! Lakini wakati yule malaika wa saba atakapotoa sauti ya tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii.”