Marko 9:1-29
Marko 9:1-29 BHN
Yesu akaendelea kuwaambia, “Kweli nawaambieni, wako wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa enzi.” Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, mavazi yake yakangaa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe. Elia na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu. Petro akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri sisi kuwapo hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema. Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni.” Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao. Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu. Basi, wakashika agizo hilo, lakini wakawa wanajadiliana wao kwa wao maana ya kufufuka kutoka kwa wafu. Wakamwuliza Yesu, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?” Naye akawajibu, “Naam, Elia anakuja kwanza kutayarisha yote. Hata hivyo, kwa nini basi imeandikwa katika Maandiko Matakatifu kwamba Mwana wa Mtu atapatwa na mateso mengi na kudharauliwa? Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyotaka kama ilivyoandikwa juu yake.” Walipowafikia wale wanafunzi wengine, waliona umati mkubwa wa watu hapo. Na baadhi ya waalimu wa sheria walikuwa wanajadiliana nao. Mara tu ule umati wa watu ulipomwona, wote walishangaa sana, wakamkimbilia wamsalimu. Yesu akawauliza, “Mnajadiliana nini nao?” Hapo mtu mmoja katika ule umati wa watu akamjibu, “Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo aliyemfanya kuwa bubu. Kila mara anapomvamia, humwangusha chini na kumfanya atokwe na povu kinywani, akisaga meno na kuwa mkavu mwili wote. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo lakini hawakuweza.” Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni kwangu.” Wakampeleka. Mara tu huyo pepo alipomwona Yesu, alimtia mtoto kifafa, naye mtoto akaanguka chini, akagaagaa na kutoka povu kinywani. Yesu akamwuliza baba yake huyo mtoto, “Amepatwa na mambo hayo tangu lini?” Naye akamjibu, “Tangu utoto wake. Na mara nyingi pepo huyo amemwangusha motoni na majini, ili amwangamize kabisa. Basi, ikiwa waweza, utuhurumie na kutusaidia!” Yesu akamwambia, “Ati ikiwa waweza! Mambo yote yanawezekana kwa mtu aliye na imani.” Hapo, huyo baba akalia kwa sauti, “Naamini! Lakini imani yangu haitoshi, nisaidie.” Yesu alipouona umati wa watu unaongezeka upesi mbele yake, alimkemea yule pepo mchafu “Pepo unayemfanya huyu mtoto kuwa bubu na kiziwi, nakuamuru, mtoke mtoto huyu wala usimwingie tena!” Hapo huyo pepo alipaza sauti, akamwangusha huyo mtoto chini, kisha akamtoka. Mtoto alionekana kama maiti, hata wengine walisema, “Amekufa!” Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama. Basi, Yesu alipoingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza kwa faragha, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?” Naye akawaambia, “Pepo wa aina hii hawezi kutoka isipokuwa kwa sala.”