Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 14:53-72

Marko 14:53-72 BHN

Basi, wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu ambapo makuhani wakuu wote, wazee na waalimu wa sheria walikuwa wamekutanika. Petro alimfuata Yesu kwa mbali, akaingia ndani ya ua wa kuhani mkuu, akaketi pamoja na walinzi akiota moto. Makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa kumshtaki Yesu wapate kumwua, lakini hawakuupata. Watu wengi walitoa ushahidi wa uongo juu ya Yesu, lakini ushahidi wao haukupatana. Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uongo wakisema: “Tulimsikia mtu huyu akisema, ‘Nitaliharibu hekalu hili lililojengwa kwa mikono, na kwa siku tatu nitajenga lingine lisilojengwa kwa mikono.’” Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukupatana. Basi, kuhani mkuu akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu, “Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?” Lakini yeye akakaa kimya; hakusema hata neno moja. Kuhani mkuu akamwuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Mtukufu?” Yesu akajibu, “Naam, mimi ndiye. Tena, mtamwona Mwana wa Mtu amekaa upande wa kulia wa yule Bwana Mwenye Nguvu, akija katika mawingu ya mbinguni.” Hapo kuhani mkuu akararua joho lake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake! Nyinyi mwaonaje?” Wote wakaamua kwamba anastahili kuuawa. Basi, baadhi yao wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, wakampiga na kumwambia, “Bashiri ni nani amekupiga!” Hata watumishi wakamchukua, wakampiga makofi. Petro alipokuwa bado chini uani, mmoja wa watumishi wa kike wa kuhani mkuu alikuja. Alipomwona Petro akiota moto, alimtazama, akamwambia, “Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.” Lakini Petro akakana, “Sijui, wala sielewi unayosema!” Kisha Petro akaondoka, akaenda nje uani. Hapo jogoo akawika. Yule mtumishi alipomwona tena Petro, akaanza tena kuwaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, “Mtu huyu ni mmoja wao.” Petro akakana tena. Baadaye kidogo, watu waliokuwa wamesimama hapo wakamwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, maana wewe ni Mgalilaya.” Lakini Petro akaanza kulaani na kuapa akisema, “Mimi simjui mtu huyu mnayesema habari zake.” Hapo jogoo akawika mara ya pili. Basi, Petro akakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Petro akabubujika machozi.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Marko 14:53-72