Marko 11:12-23
Marko 11:12-23 BHN
Kesho yake, walipokuwa wanatoka Bethania, Yesu aliona njaa. Basi, akaona kwa mbali mtini wenye majani mengi. Akauendea ili aone kama ulikuwa na tunda lolote. Alipoufikia, aliukuta bila tunda lolote ila tu majani matupu, kwa vile hayakuwa majira yake ya matunda. Hapo akauambia mtini, “Tangu leo hata milele mtu yeyote asile matunda kwako.” Nao wanafunzi wake walisikia maneno hayo. Basi, wakafika Yerusalemu. Yesu akaingia hekaluni akaanza kuwafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilishana fedha, na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. Hakumruhusu mtu yeyote kupitia hekaluni akichukua kitu. Kisha akawafundisha, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa ajili ya mataifa yote!’ Lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyanganyi!” Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake. Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini. Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi. Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!” Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu. Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo.