Mathayo 8:18-27
Mathayo 8:18-27 BHN
Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ngambo ya ziwa. Mwalimu mmoja wa sheria akamwendea, akamwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata kokote utakakokwenda.” Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.” Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu.” Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao.” Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye. Mara, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu lakini alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, “Bwana, tuokoe, tunaangamia!” Yesu akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?” Basi, akainuka, akaukemea upepo na lile ziwa; kukawa shwari kabisa. Watu wakashangaa, wakasema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na bahari vinamtii!”