Mathayo 27:27-46
Mathayo 27:27-46 BHN
Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu. Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!” Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani. Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha. Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu. Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa, wakampa mchanganyiko wa divai na kitu kichungu. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa. Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Wakaketi, wakawa wanamchunga. Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lililoandikwa, “Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.” Wanyanganyi wawili walisulubiwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!” Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria na wazee walimdhihaki wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini. Alimtumainia Mungu na kusema ati yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka.” Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana. Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, giza likaikumba nchi yote. Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”