Mathayo 22:15-33
Mathayo 22:15-33 BHN
Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake. Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako. Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?” Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu? Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha. Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao. Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu. Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake.