Mathayo 17:1-13
Mathayo 17:1-13 BHN
Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, uso wake ukangaa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama mwanga. Mose na Elia wakawatokea, wakawa wanazungumza naye. Hapo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Alipokuwa bado anasema hivyo, wingu jeupe likawafunika, na sauti ikasikika kutoka hilo wingu: “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni.” Wanafunzi waliposikia hivyo wakaanguka kifudifudi, wakaogopa sana. Yesu akawaendea, akawagusa, akasema, “Simameni, msiogope!” Walipoangalia juu hawakumwona mtu, ila Yesu peke yake. Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu akawaonya: “Msimwambie mtu mambo mliyoyaona mpaka Mwana wa Mtu atakapofufuliwa kutoka wafu.” Kisha wanafunzi wakamwuliza, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?” Yesu akawajibu, “Kweli, Elia atakuja kutayarisha mambo yote. Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja nao hawakumtambua, bali walimtendea jinsi walivyotaka. Mwana wa Mtu atateswa vivyo hivyo mikononi mwao.” Hapo hao wanafunzi wakafahamu kwamba alikuwa akiwaambia juu ya Yohane Mbatizaji.