Mathayo 12:38-45
Mathayo 12:38-45 BHN
Kisha baadhi ya waalimu wa sheria na Mafarisayo wakamwambia Yesu, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.” Naye akawajibu, “Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara, lakini hamtapewa ishara isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. Jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha. Watu wa Ninewi watatokea wakati wa hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Yona! Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali, akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Solomoni. “Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika asipate. Hapo hujisemea: ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka’. Lakini anaporudi na kuikuta tupu, imefagiwa na kupambwa, huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye; na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu.”