Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 10:5-15

Mathayo 10:5-15 BHN

Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: “Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika miji ya Wasamaria. Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. Mnapokwenda hubirini hivi: ‘Ufalme wa mbinguni umekaribia.’ Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake. “Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu anayestahili kutembelewa, na kaeni huko mpaka mtakapoondoka mahali hapo. Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. Kama wenyeji wa nyumba hiyo wanastahili salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawastahili, basi amani yenu itawarudia nyinyi. Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakunguteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. Kweli nawaambieni, siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora.