Luka 8:26-40
Luka 8:26-40 BHN
Wakaendelea na safari, wakafika pwani ya nchi ya Wagerase inayokabiliana na Galilaya, ngambo ya ziwa. Alipokuwa anashuka pwani, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo alimjia kutoka mjini. Kwa muda mrefu mtu huyo hakuwa anavaa nguo, wala hakuwa anaishi nyumbani bali makaburini. Alipomwona Yesu, alijitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kubwa, “We, Yesu Mwana wa Mungu Mkuu, una shauri gani nami? Ninakusihi usinitese!” Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia huyo pepo mchafu amtoke mtu huyo. Pepo huyo mchafu alikuwa anamvamia mtu huyo mara nyingi, na ingawa watu walimweka ndani na kumfunga kwa minyororo na pingu, lakini kila mara alivivunja vifungo hivyo, akakimbizwa na pepo huyo mchafu hadi jangwani. Basi, Yesu akamwuliza, “Jina lako nani?” Yeye akajibu, “Jina langu ni ‘Jeshi’” – kwa sababu pepo wengi walikuwa wamempagaa. Hao pepo wakamsihi asiwapeleke kwenye shimo kuu. Mahali hapo kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha mlimani. Basi, hao pepo wakamsihi awaruhusu wawaingie. Naye Yesu akawapa ruhusa. Kwa hiyo pepo hao wakamtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nao wakaporomoka kwenye ule mteremko mkali, wakatumbukia ziwani, wakafa maji. Wale wachungaji walipoona yote yaliyotokea walikimbia, wakaenda kuwapa watu habari mjini na mashambani. Watu wakaja kuona yaliyotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mtu aliyetokwa na pepo ameketi karibu na Yesu, amevaa nguo, ana akili zake, wakaogopa. Wale watu walioshuhudia tukio hilo waliwaeleza hao jinsi yule mtu alivyoponywa. Wakazi wa nchi ya Gerase walishikwa na hofu kubwa. Kwa hiyo wakamwomba Yesu aondoke, aende zake. Hivyo Yesu alipanda tena mashua, akaondoka. Yule mtu aliyetokwa na wale pepo akamsihi aende pamoja naye. Lakini Yesu hakumruhusu, bali akamwambia, “Rudi nyumbani ukaeleze yote Mungu aliyokutendea.” Basi, yule mtu akaenda akitangaza kila mahali katika mji ule mambo yote Yesu aliyomtendea. Yesu aliporudi upande mwingine wa ziwa, kundi la watu lilimkaribisha, kwa maana wote walikuwa wanamngojea.