Luka 22:7-23
Luka 22:7-23 BHN
Basi, siku ya mikate isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa. Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, “Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka.” Nao wakamwuliza, “Unataka tuiandae wapi?” Akawaambia, “Sikilizeni! Mtakapokuwa mnakwenda mjini, mtakutana na mwanamume anayebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka ndani ya nyumba atakayoingia. Mwambieni mwenye nyumba: ‘Mwalimu anakuuliza, kiko wapi kile chumba ambamo nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?’ Naye atawaonesheni chumba kikubwa ghorofani ambacho kimepambwa. Andalieni humo.” Basi, wakaenda, wakakuta kila kitu sawa kama Yesu alivyokuwa amewaambia; wakaandaa karamu ya Pasaka. Saa ilipotimia, Yesu akakaa kula chakula pamoja na mitume wake. Akawaambia, “Nimetamani sana kula Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. Maana nawaambieni, sitaila tena hadi hapo itakapokamilika katika ufalme wa Mungu.” Kisha akatwaa kikombe cha divai, akashukuru, akasema, “Pokeeni, mgawane. Kwa maana nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka ufalme wa Mungu utakapokuja.” Halafu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka.” Akafanya vivyo hivyo na kikombe cha divai baada ya chakula, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu inayomwagika kwa ajili yenu. “Lakini, tazameni! Yule atakayenisaliti yuko nami hapa mezani. Kweli Mwana wa Mtu anakwenda kuuawa kama ilivyopangwa, lakini ole wake mtu anayemsaliti.” Hapo wakaanza kuulizana wao kwa wao ni nani kati yao atakayefanya jambo hilo.