Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 12:1-34

Luka 12:1-34 BHN

Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa. Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonongona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba. “Nawaambieni nyinyi rafiki zangu: Msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi. Nitawaonesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo. Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa sarafu ndogo kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi; nyinyi mna thamani kuliko shomoro wengi! “Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake. Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. “Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. “Watakapowapeleka nyinyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala, msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema. Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema.” Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba.” Yesu akamjibu, “Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au msuluhishi kati yenu?” Basi, akawaambia wote, “Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uhai wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo.” Kisha akawaambia mfano: “Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi. Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: ‘Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu? Nitafanya hivi: Nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, nami nitahifadhi humo mavuno yangu yote na mali yangu. Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: Sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, kula, kunywa na kufurahi.’ Lakini Mungu akamwambia: ‘Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojirundikia vitakuwa vya nani?’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejirundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu.” Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. Chukueni kwa mfano, kunguru: Hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Nyinyi mna thamani zaidi kuliko ndege! Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuongeza kidogo urefu wa maisha yake? Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. Ikiwa basi, Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, si atawafanyia nyinyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! “Basi, msivurugike akili, mkihangaika juu ya mtakachokula au mtakachokunywa. Kwa maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wote wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo. Shughulikeni kwanza juu ya ufalme wa Mungu, na hayo mtapewa kwa ziada. “Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme. Uzeni mali yenu mkawape maskini hizo fedha. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na kujiwekea hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu. Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.