Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 24:1-15

Yoshua 24:1-15 BHN

Kisha Yoshua akayakusanya makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maofisa wa Israeli, nao wakaja mbele ya Mungu. Yoshua akawaambia watu wote, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Hapo zamani, wazee wenu waliishi ngambo ya mto Eufrate, wakaitumikia miungu mingine. Mzee mmoja alikuwa Tera, baba yao Abrahamu na Nahori. Mimi Mungu nilimwondoa babu yenu Abrahamu kutoka huko ngambo ya mto Eufrate na kumleta hapa Kanaani, ambako nilimpatia wazawa wengi. Nilimpa Isaka, naye Isaka nikampa Yakobo na Esau. Nilimpa Esau milima ya Seiri aimiliki. Lakini Yakobo na watoto wake walikwenda Misri. Baadaye niliwatuma Mose na Aroni, nikailetea nchi ya Misri mapigo, na baadaye nikawatoa nyinyi nchini humo. Niliwatoa wazee wenu kutoka Misri na kuwaleta hadi kwenye bahari ya Shamu. Wamisri waliwafuatia wakiwa na magari na askari wapandafarasi. Waisraeli waliponililia mimi Mwenyezi-Mungu, niliweka giza kati yao na Wamisri na kuifanya bahari iwafunike Wamisri. Nyinyi wenyewe mlijionea yale niliyowatendea Wamisri. Mliishi jangwani muda mrefu. Kisha niliwaongoza hadi katika nchi ya Waamori ambao waliishi upande mwingine wa mto Yordani. Walipigana nanyi, lakini mimi niliwapeni ushindi juu yao mkawaangamiza na kuiteka nchi yao. Naye Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akaja na kuwashambulia Waisraeli. Akamwalika Balaamu mwana wa Beori aje kuwalaani nyinyi. Lakini mimi sikumsikiliza Balaamu, naye ikambidi kuwabariki, nami nikawaokoa nyinyi mikononi mwa Balaki. Halafu mkavuka mto Yordani, mkafika Yeriko. Wakazi wa Yeriko walipigana nanyi, hali kadhalika na Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi. Hao mimi nikawatia mikononi mwenu. Nilituma manyigu mbele yenu ambayo yaliwatimua wafalme wawili wa Waamori. Hamkufanya haya kwa kupania mapanga wala pinde zenu. “Niliwapeni mashamba ambayo hamkuwa mmeyalima, na miji ambayo hamkuijenga ambamo sasa mnaishi, na kula matunda ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuipanda. “Sasa, basi, mcheni Mwenyezi-Mungu na kumtumikia kwa moyo mnyofu na uaminifu. Acheni kabisa miungu ile ambayo wazee wenu waliiabudu ngambo ya mto Eufrate na nchini Misri. Mtumikieni Mwenyezi-Mungu. Kama hamtaki kumtumikia Mwenyezi-Mungu, basi chagueni leo hii ni nani mtakayemtumikia: Kwamba ni miungu ile ambayo wazee wenu waliitumikia ngambo ya mto Eufrate, au miungu ya Waamori ambao sasa mnaishi nchini mwao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu.”

Soma Yoshua 24