Yona 3:1-10
Yona 3:1-10 BHN
Neno la Mwenyezi-Mungu likamjia Yona mara ya pili: “Nenda Ninewi, ule mji mkuu, ukawatangazie watu ujumbe niliokupa.” Basi, Yona akaondoka, akaenda Ninewi kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza. Mji wa Ninewi ulikuwa mkubwa sana. Upana wake ulikuwa mwendo wa siku tatu. Alipowasili, Yona aliingia mjini, na baada ya kutembea mwendo wa siku nzima, akaanza kutangaza: “Bado siku arubaini tu na mji huu wa Ninewi utaangamizwa!” Basi, watu wa Ninewi wakauamini ujumbe wa Mungu, wakatangaza mfungo, na kwamba kila mmoja wao, mkubwa kwa mdogo, avae vazi la gunia kama ishara ya kutubu. Habari hizi zikamfikia mfalme wa Ninewi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake rasmi, akajivika vazi la gunia na kuketi katika majivu. Kisha mfalme akawatangazia wakazi wa Ninewi: “Mimi mfalme, pamoja na wakuu wangu, natoa amri hii: Pasiwe na binadamu yeyote, ng'ombe au mnyama yeyote wa kufugwa, atakayeonja kitu chochote. Ni mwiko kwa mtu yeyote au mnyama kula au kunywa. Watu wote na wanyama wavae mavazi ya gunia. Kila mtu na amwombe Mungu na kumsihi kwa moyo. Naam, kila mmoja na aache uovu na ukatili wake. Huenda Mungu akabadili nia yake, akaacha kutukasirikia, tusije tukaangamia!” Mungu alipoona walivyofanya, na jinsi walivyouacha uovu wao, akabadili nia yake, akaacha kuwatenda kama alivyokuwa amekusudia.