Yobu 34:16-30
Yobu 34:16-30 BHN
“Kama una akili sikiliza; sikiliza ninachokuambia. Je, anayetawala ulimwengu kwa sheria zake anachukia haki? Je, utathubutu kumhukumu mwadilifu na mwenye nguvu? Amwambiaye mfalme, ‘Wewe ni takataka!’ Na watu mashuhuri, ‘Nyinyi ni waovu!’ Yeye hawapendelei wakuu, wala kuwajali matajiri kuliko maskini, maana wote hao ni kazi ya mikono yake. Kufumba na kufumbua hao wamekufa; hutikiswa usiku na kuaga dunia; nao wenye nguvu hufutiliwa mbali bila kutumia nguvu za mtu. “Macho ya Mungu huchunguza mienendo ya watu; yeye huziona hatua zao zote. Hakuna weusi wala giza nene ambamo watenda maovu waweza kujificha. Mungu hahitaji kumjulisha mtu wakati wa kumleta mbele ya mahakama yake. Huwaangamiza wenye nguvu bila uchunguzi, na kuwaweka wengine mahali pao. Kwa kuwa anayajua matendo yao yote, huwaporomosha usiku wakaangamia. Huwachapa hadharani kwa ajili ya uovu wao, kwa sababu wameacha kumfuata yeye, wakazipuuza njia zake zote. Hata wakasababisha kilio cha maskini kimfikie Mungu, Mungu akasikiliza kilio chao hao walioteswa. Kama Mungu akinyamaza, nani awezaye kumlaumu? Kama akificha uso wake, nani awezaye kumwona, liwe ni taifa au mtu mmojammoja? Hufanya hivyo, mtu mbaya asitawale, au wale wahatarishao maisha ya watu.