Yohane 5:30-47
Yohane 5:30-47 BHN
“Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi ninahukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma. Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli. Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli. Nyinyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli. Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa. Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo. Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma. Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Nyinyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake, na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma. Nyinyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uhai wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia! Hata hivyo, nyinyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uhai. “Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu. Lakini nawajua nyinyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu. Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea. Mwawezaje kuamini, hali nyinyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu nyinyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu? Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye nyinyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki. Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia, maana Mose aliandika juu yangu. Lakini hamyaamini yale aliyoandika; mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?”