Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohane 19:28-42

Yohane 19:28-42 BHN

Kisha, Yesu aliona kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, “Naona kiu.” Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni. Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, “Yametimia!” Kisha akainamisha kichwa, akatoa roho. Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe. Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu. Lakini walipomfikia Yesu, waliona kwamba alikwisha kufa, kwa hivyo hawakumvunja miguu. Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji. ( Naye aliyeona tukio hilo ameshuhudia ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli). Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: “Hapana hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.” Tena Maandiko mengine yanasema: “Watamtazama yule waliyemtoboa.” Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Arimathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi). Basi, Pilato akamruhusu. Hivyo Yosefu alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu. Naye Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani kiasi cha kilo thelathini. Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana na desturi ya Wayahudi katika kuzika. Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo kulikuwa na kaburi jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake. Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha