Yohane 11:45-57
Yohane 11:45-57 BHN
Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu, wakamwamini. Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu. Kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza Kuu, wakasema, “Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno. Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu hekalu letu na taifa letu!” Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, akawaambia, “Nyinyi hamjui kitu! Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?” Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao; na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika. Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu. Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake. Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo. Basi, wakawa wanamtafuta Yesu. Nao walipokusanyika pamoja hekaluni, wakaulizana, “Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au sivyo?” Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba mtu akijua mahali aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni.