Yakobo 3:2-13
Yakobo 3:2-13 BHN
Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni mkamilifu, na anaweza kutawala nafsi yake yote. Sisi huwatia farasi lijamu kinywani mwao ili watutii; na kwa njia hiyo twaweza kuwaongoza kokote tunakotaka. Meli nazo pia, ingawa ni kubwa sana, na husukumwa na upepo mkali, huweza kugeuzwa kwa usukani mdogo sana, zikaelekea kokote nahodha anakotaka. Vivyo hivyo, ulimi, ingawa ni kiungo kidogo cha mwili, hujisifia makuu sana. Moto mdogo waweza kuteketeza msitu mkubwa. Hali kadhalika ulimi ni kama moto. Umejaa maovu chungu nzima, unayo nafasi yake katika miili yetu na hueneza ubaya katika nafsi zetu zote. Huteketeza maisha yetu yote kwa moto utokao Jehanamu kwenyewe. Binadamu anaweza kuwafuga wanyama, na amefaulu kufuga viumbe vyote – wanyama wa mwituni, ndege, nyoka na viumbe vya baharini. Lakini hakuna mtu aliyefaulu kuufuga ulimi. Ulimi ni kitu kiovu, hakitawaliki, na kimejaa sumu inayoua. Kwa ulimi sisi twamshukuru Bwana na Baba yetu. Kwa ulimi huhuo twawalaani watu, watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Maneno ya kubariki na ya kulaani hutoka katika kinywa kimoja. Ndugu zangu, mambo haya hayapaswi kuwa hivyo. Je, chemchemi moja yaweza kutoa maji matamu na maji machungu pamoja? Ndugu zangu, je, mtini waweza kuzaa zeituni? Au, mzabibu waweza kuzaa tini? Chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu. Je, ni nani mwenye hekima na akili miongoni mwenu? Basi, aoneshe jambo hilo kwa mwenendo wake mzuri na kwa matendo yake mema yanayofanyika kwa unyenyekevu na hekima.