Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 24:48-67

Mwanzo 24:48-67 BHN

Kisha nikainama na kumwabudu Mwenyezi-Mungu; nikamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye ameniongoza moja kwa moja kwa binti wa ukoo wa bwana wangu kwa ajili ya mwanawe. Sasa, basi, niambieni kama mko tayari kumtendea bwana wangu kwa uaminifu na haki; kama sivyo, basi semeni, nami nitajua cha kufanya.” Baada ya kusikia hayo, Labani na Bethueli wakamjibu, “Jambo hili limetoka kwa Mwenyezi-Mungu, sisi hatuwezi kuamua lolote. Rebeka huyu hapa; mchukue uende. Na awe mke wa mwana wa bwana wako kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.” Mtumishi wa Abrahamu aliposikia maneno hayo, alimsujudia Mwenyezi-Mungu. Kisha akatoa vito vya fedha na dhahabu na nguo, akampa Rebeka. Pia aliwapa ndugu na mama yake Rebeka mapambo ya thamani kubwa. Mtumishi wa Abrahamu na watu aliokuja nao wakala, wakanywa na kulala huko. Walipoamka asubuhi, mtumishi yule akasema, “Naomba kurudi kwa bwana wangu.” Lakini ndugu na mama yake Rebeka wakasema, “Mwache msichana akae nasi muda mfupi, kama siku kumi hivi; kisha anaweza kwenda.” Lakini yeye akasema, “Tafadhali, msinicheleweshe, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha fanikisha safari yangu; naomba mniruhusu kurudi kwa bwana wangu.” Nao wakasema, “Basi, tumwite msichana mwenyewe, tumwulize.” Wakamwita Rebeka na kumwuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?” Naye akajibu, “Nitakwenda.” Basi, wakamwacha Rebeka na yaya wake aende na mtumishi wa Abrahamu na watu wake. Yaya wake Rebeka pia aliandamana naye. Basi, wakambariki Rebeka wakisema, “Ewe dada yetu! Uwe mama wa maelfu kwa maelfu; wazawa wako waimiliki miji ya adui zao.” Kisha, Rebeka na wajakazi wake wakapanda ngamia na kumfuata huyo mtumishi wa Abrahamu; nao wote wakaondoka. Wakati huo, Isaka alikuwa ameondoka Beer-lahai-roi, akawa anakaa huko pande za Negebu. Siku moja jioni, Isaka alikwenda mashambani kutafakari. Basi, akatazama akaona ngamia wanakuja. Naye Rebeka alipotazama na kumwona Isaka, alishuka chini na kumwuliza mtumishi wa Abrahamu, “Ni nani yule mtu anayetembea kule shambani, anakuja kutulaki?” Yule mtumishi akasema, “Ni bwana wangu.” Basi, Rebeka akatwaa shela yake, akajifunika uso. Yule mtumishi akamsimulia Isaka yote aliyokuwa ameyafanya. Basi, Isaka akamchukua Rebeka ndani ya hema iliyokuwa ya Sara mama yake, akawa mke wake. Isaka akampenda Rebeka na kupata faraja baada ya kifo cha mama yake.

Soma Mwanzo 24

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mwanzo 24:48-67