Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 43:13-27

Ezekieli 43:13-27 BHN

Vipimo vya madhabahu, vitakuwa vilevile kama vipimo vya hekalu. Kuuzunguka msingi wa madhabahu, kutakuwa na mfereji wenye kina cha sentimita 50 na upana wa sentimita 50, pamoja na ukingo wenye kina cha sentimita 25. Sehemu ya madhabahu itakayokuwa chini kabisa tokea juu ya msingi itakuwa na kimo cha mita 1. Sehemu itakayofuata itawekwa nyuma kutoka kwenye ukingo sentimita 50 kuzunguka, na kimo cha mita 2. Sehemu itakayofuata nayo itawekwa nyuma ya ukingo sentimita 50 kuzunguka. Sehemu hii ya juu, ambayo itatumika kuteketezea sadaka, itakuwa mraba, kila upande mita 2. Mjengo wa kona za sehemu hii ya juu zitainuka kuliko sehemu nyingine. Sehemu ya juu ya madhabahu itakuwa mraba, mita 6 kila upande. Sehemu ya katikati, itakuwa mraba, sentimita 7 kila upande, nayo itakuwa na ukingo pembeni wenye kimo cha sentimita 25. Kutakuwa na mfereji wenye upana wa sentimita 50. Na kutakuwa na vidato vya kupandia madhabahu upande wa mashariki. Bwana Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wakati madhabahu imejengwa, utaiweka wakfu kwa kutoa tambiko za kuteketezwa juu yake na kuinyunyizia damu ya wanyama waliotolewa sadaka. Wale makuhani walio wa kabila la Lawi ambao ni wazawa wa Sadoki, ndio tu watakaonikaribia ili kunihudumia. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Utawapa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuondoa dhambi. Utatwaa damu yake na kuitia juu ya pembe nne za madhabahu na juu ya ncha nne za daraja na juu ya pambizo yake pande zote. Hivyo ndivyo utakavyoitakasa madhabahu na kuiweka wakfu. Utachukua pia fahali wa sadaka ya kuondoa dhambi; watamteketeza katika mahali palipochaguliwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, lakini nje ya mahali patakatifu. Kesho yake, utatoa beberu asiye na dosari, kuwa sadaka ya kuondoa dhambi; madhabahu itatakaswa kama ilivyotakaswa kwa damu ya fahali. Utakapokwisha kuitakasa, utatwaa fahali mdogo asiye na dosari na kondoo dume mmoja asiye na dosari na kuwaleta mbele yangu. Makuhani watawapaka chumvi na kuwatoa kuwa tambiko ya kuteketezwa, kwa Mwenyezi-Mungu. Kwa muda wa siku saba, kila siku utatambika beberu mmoja awe sadaka ya kuondoa dhambi. Pia watatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja asiye na dosari. Hivyo kwa muda wa siku saba, utafanya upatanisho na kuitakasa, na hivyo kuiweka wakfu madhabahu. Baada ya siku hizo saba, tokea siku ya nane na kuendelea, makuhani watatoa sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani. Nami nitawakubali. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”