Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 25:10-30

Kutoka 25:10-30 BHN

“Waisraeli watengeneze sanduku la mbao za mjohoro, lenye urefu wa sentimita 110, upana sentimita 66, na kimo sentimita 66. Utalipaka sanduku hilo dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu pande zote. Kisha utalitengenezea pete nne na kuzitia miguuni pake, kila mguu pete moja. Utatengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu. Mipiko hiyo utaipitisha katika pete zilizo pande mbili za sanduku, kwa ajili ya kulibebea. Mipiko hiyo itabaki daima katika pete; isitolewe wakati wowote. Ndani ya sanduku hilo utaweka vibao viwili vya mawe vya ushuhuda. “Kisha utatengeneza kwa dhahabu safi kiti cha rehema, urefu wake sentimita 110, na upana wake sentimita 66. Utatengeneza pia mfano wa viumbe hai viwili kwa kufua dhahabu, uviweke kwenye miisho miwili ya kiti hicho; kiumbe kimoja mwisho mmoja na kiumbe kingine mwisho mwingine. Viweke viumbe hivyo kwenye miisho ya kiti hicho, lakini viwe kitu kimoja na hicho kiti. Viumbe hivyo vitaelekeana, mabawa yake yamekunjuka kukifunika kiti cha rehema; nyuso zake zitaelekea kiti hicho. Ndani ya sanduku utaweka vibao viwili vya mawe na kukiweka kiti cha rehema juu yake. Mimi nitakutana nawe hapo; na kutoka juu ya kiti hicho cha rehema katikati ya viumbe hao walioko juu ya sanduku la ushuhuda, nitazungumza nawe na kukupa amri zote kwa ajili ya Waisraeli. “Utatengeneza meza ya mbao za mjohoro yenye urefu wa sentimita 88, upana sentimita 44 na kimo sentimita 66. Hiyo meza utaipaka dhahabu safi na kuizungushia utepe wa dhahabu. Kisha utaizungushia ubao wenye upana wa sentimita 66. Utaitengenezea pete nne za dhahabu na kuzitia kwenye pembe zake miguuni pake. Pete hizo zitakuwa karibu na ule ubao wa kuizunguka meza na zitakuwa za kushikilia mipiko ya kuibebea hiyo meza. Utatengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu; mipiko itakuwa ya kuibebea hiyo meza. Utatengeneza sahani na vikombe vya kuwekea ubani mezani, na pia bilauri na bakuli za kumiminia tambiko za kinywaji. Vifanye vyombo hivyo vyote kwa dhahabu safi. Meza hiyo utaiweka mbele ya sanduku la agano, na juu ya meza hiyo utaiweka ile mikate ya kuwekwa mbele yangu daima.

Soma Kutoka 25