Waefeso 4:17-32
Waefeso 4:17-32 BHN
Basi, kwa jina la Bwana, nawaonyeni: Msiishi tena kama watu wasiomjua Mungu, ambao fikira zao zimekuwa upuuzi mtupu, na akili zao zimo gizani. Wako mbali na uhai wa Mungu kwa sababu ya upumbavu ulio ndani yao na ukaidi wao. Wamepotoka na hawana aibu, wamejitosa katika ufisadi; hufanya kwa pupa kila aina ya mambo ya aibu. Lakini nyinyi hamkujifunza hivyo juu ya Kristo. Ni dhahiri kwamba mlisikia barabara habari zake, na mkiwa wafuasi wake mkafundishwa ukweli ulivyo katika Yesu. Basi, acheni mwenendo wenu wa awali, yaani ule utu wenu wa kale uliokuwa unaangamizwa kwa tamaa zake danganyifu. Jirekebisheni upya rohoni na katika fikira zenu. Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu. Kwa hiyo, acheni uongo. Kila mmoja anapaswa kumwambia mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo. Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima. Msimpe Ibilisi nafasi. Aliyekuwa akiiba, asiibe tena, bali na aanze kufanya kazi njema kwa mikono yake, apate kuwa na kitu cha kumsaidia mtu aliye maskini. Maneno mabaya hata yasisikike kamwe miongoni mwenu; kila mara maneno yenu yawe ya kufaa na ambayo hujenga na kuwasaidia wengine, ili yawaneemeshe wasikilizaji wenu. Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, maana Roho huyo ni alama ya Mungu kwenu kwamba nyinyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku itakuja ambapo Mungu atawakomboeni. Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele na matusi. Acheni kila uovu! Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe nyinyi kwa njia ya Kristo.