Danieli 11:5-20
Danieli 11:5-20 BHN
“ ‘Mfalme wa kusini atakuwa mwenye nguvu. Lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu kuliko yeye na utawala wake utakuwa mkubwa zaidi. Baada ya miaka kadhaa, watafanya mkataba; binti mfalme wa kusini ataolewa katika jamaa ya mfalme na kuratibisha huo mkataba; wa kaskazini, lakini hataendelea kuwa na nguvu, pia mfalme na wazawa wake hawatavumilia; na huyo binti, mwanawe na watumwa wa kike aliokwenda nao, wote watauawa. Baadaye, mmojawapo wa ukoo wa huyo binti atakuwa mfalme. Huyo atayashambulia majeshi ya mfalme wa kaskazini na kuingia katika ngome zao na kushinda. Atazibeba sanamu za kusubu za miungu yao na vyombo vya thamani vya fedha na dhahabu mpaka nchini Misri. Kwa muda wa miaka kadhaa, mfalme wa kusini hatamshambulia mfalme wa kaskazini. Lakini baadaye, mfalme huyu wa kaskazini atauvamia ufalme wa kusini, ila atalazimika kurudi katika nchi yake. “ ‘Wana wa mfalme wa kaskazini watakusanya jeshi kubwa na kujiandaa kwa vita. Jeshi hilo litasonga mbele kama mafuriko litapita na kupigana vita mpaka ngome ya adui. Hapo, mfalme wa kusini, kwa hasira yake, atapigana vita na mfalme wa kaskazini ambaye naye atamkabili kwa jeshi kubwa, lakini litashindwa. Baada ya kulishinda vibaya jeshi la kaskazini na kuua maelfu, ataanza kujisifu, ila hataendelea kuwa mshindi. “ ‘Maana mfalme wa kaskazini baadaye ataandaa jeshi kubwa kuliko lile la awali. Kisha baada ya miaka kadhaa atarudi na jeshi kubwa lenye vifaa vingi. Wakati huo watu wengi watamwasi mfalme wa kusini. Baadhi ya watu wakatili wa taifa lako Danieli, wataasi ili kutekeleza maono haya, lakini hawatafaulu. Ndipo mfalme wa kaskazini atauzingira mji wenye ngome imara na kuuteka. Wanajeshi wa kusini hawatastahimili, hata wale wateule, maana hawatakuwa na nguvu. Mvamizi atawatenda kama apendavyo, hakuna atakeyethubutu kupingana naye. Atasimama katika nchi tukufu, na nchi hiyo yote itakuwa chini ya mamlaka yake. “ ‘Huyo mvamizi atakusudia kuja na jeshi lake lote, naye atafanya mapatano na kuyatekeleza. Atamwoza binti mmoja ili kuuangamiza ufalme wa adui yake; lakini mpango wake hautafaulu, wala kumfaidia lolote. Baadaye, atazigeukia na kuzishambulia nchi nyingi za pwani na kuzishinda. Lakini jemadari mgeni atamshinda na kuyakomesha majivuno yake mwenyewe; naam, atamrudishia mfalme wa kaskazini majivuno yake mwenyewe. Hapo atageuka kurudi katika ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka vitani na huo ndio utakaokuwa mwisho wake. “ ‘Huyu atafuatwa na mfalme mwingine ambaye atatuma mtozaushuru kupitia katika fahari ya ufalme wake. Mfalme huyo atauawa baada ya siku chache, lakini si kwa hasira wala vitani.