Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 18:14-27

2 Mambo ya Nyakati 18:14-27 BHN

Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme akamwuliza, “Je, twende kupigana vitani huko Ramoth-gileadi au nisiende?” Mikaya akajibu, “Nenda ushinde; Mwenyezi-Mungu atawatia mikononi mwako.” Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba kila unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?” Naye Mikaya akasema, “Niliwaona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; waache warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’” Hapo mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia, kamwe hatatabiri jema juu yangu, ila mabaya tu?” Kisha Mikaya akasema: “Haya, sikia neno la Mwenyezi-Mungu: Nilimwona Mwenyezi-Mungu ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lake lote la mbinguni limesimama upande wake wa kulia na wa kushoto. Ndipo Mwenyezi-Mungu akauliza, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu mfalme wa Israeli aende akaangamie huko Ramoth-gileadi?’ Kila mmoja akajibu alivyofikiri. Kisha, pepo mmoja akajitokeza mbele ya Mwenyezi-Mungu, akasema, ‘Mimi nitamshawishi.’ Mwenyezi-Mungu akamwuliza, ‘Kwa mbinu gani?’ Naye akajibu, ‘Nitakwenda na kuwafanya manabii wake wote waseme uongo.’ Mwenyezi-Mungu akamwambia, ‘Wewe utamshawishi na utafaulu; haya nenda ukafanye hivyo.’ Basi ndivyo ilivyo: Mwenyezi-Mungu amewafanya hawa manabii wako waseme uongo. Lakini Bwana amenena mabaya juu yako!” Hapo nabii Sedekia mwana wa Kenaana akamkaribia Mikaya, akampiga kofi shavuni na kumwuliza, “Kwa njia gani Roho wa Mwenyezi-Mungu ameniacha na akaja kunena nawe?” Mikaya akamjibu, “Siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani kujificha ndipo utakapojua.” Naye mfalme wa Israeli akatoa amri, “Mkamateni Mikaya mrudisheni kwa Amoni, mkuu wa mji, na kwa Yoashi, mwana wa mfalme. Waambie wamfunge gerezani na kumlisha mkate kidogo na maji, mpaka nitakaporudi salama.” Ndipo Mikaya aliposema, “Ukirudi salama, basi, utajua Mwenyezi-Mungu hakunena nami.” Kisha akaendelea kusema, “Sikieni, enyi watu wote!”