1 Petro 5:1-11
1 Petro 5:1-11 BHN
Mimi mzee miongoni mwenu wazee wenzangu, mimi ambaye nilishuhudia mateso ya Kristo na kushiriki ule utukufu utakaofunuliwa, nawasihini mlichunge lile kundi la Mungu mlilokabidhiwa; mlitunze si kwa kulazimika, bali kwa hiari kama atakavyo Mungu. Fanyeni kazi hiyo si kwa tamaa ya fedha, bali kwa moyo wenu wote. Msiwatawale kwa mabavu hao waliowekwa chini ya ulinzi wenu, bali muwe mfano kwa hilo kundi. Na wakati Mchungaji Mkuu atakapotokea, nyinyi mtapokea taji ya utukufu isiyofifia. Kadhalika nanyi vijana mnapaswa kujiweka chini ya mamlaka ya wazee. Nyinyi nyote mnapaswa kuwa na unyenyekevu mpate kutumikiana; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Mungu huwapinga wenye majivuno, lakini huwajalia neema wanyenyekevu.” Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa enzi wa Mungu, ili awainue wakati ufaao. Mwekeeni matatizo yenu yote, maana yeye anawatunzeni. Muwe macho; kesheni! Maana adui yenu, Ibilisi, huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mawindo. Muwe imara katika imani na kumpinga, mkijua kwamba ndugu zenu pote duniani wanapatwa na mateso hayohayo. Lakini mkisha teseka muda mfupi, Mungu aliye asili ya neema yote na ambaye anawaiteni kuushiriki utukufu wake wa milele katika kuungana na Kristo, yeye mwenyewe atawakamilisheni na kuwapeni uthabiti, nguvu na msingi imara. Kwake yawe mamlaka milele! Amina.