Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 8:41-53

1 Wafalme 8:41-53 BHN

“Vivyo hivyo, wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli akija kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako (maana watu wa mataifa mengine watasikia sifa zako na kuhusu nguvu na uwezo wako), mtu huyo akija na kuomba katika nyumba hii, nakusihi umsikie kutoka huko mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba; kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako, Israeli, na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga, inajulikana kwa jina lako. “Watu wako wakienda vitani kupigana na adui yao kokote kule utakakowapeleka, nao wakikuomba wakielekea mji uliouchagua na nyumba niliyoijenga kwa ajili ya jina lako, nakusihi usikie sala yao na maombi yao huko mbinguni, uwapatie ushindi vitani. “Ikiwa watatenda dhambi dhidi yako maana hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukiwakasirikia na kuwaacha washindwe na adui, hata wapelekwe mateka mpaka nchi ya adui iliyoko mbali au karibu; kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi moyoni na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu;’ pia wakati huo watakapokuwa katika nchi ya adui zao, wakitubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, wakielekea mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako, basi, nakusihi kutoka huko mbinguni uliko usikie sala yao na ombi lao uwapatie haki zao. Uwasamehe watu wako dhambi walizotenda dhidi yako na uasi wao, uwahurumie mbele ya adui zao, ili nao wapate kuwahurumia, maana ni watu wako, na ni mali yako; watu ambao uliwatoa Misri kutoka katika tanuri ya chuma. “Uangalie ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako, Israeli, uwasikie kila wanapokuomba. Kwa sababu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu uliwatenga na watu wa mataifa mengine duniani, ili wawe mali yako – kama ulivyotangaza kwa njia ya Mose, mtumishi wako, wakati ule ulipowatoa babu zetu katika nchi ya Misri.”