Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:11-21

1 Wafalme 1:11-21 BHN

Hapo, Nathani akamwendea Bathsheba mama yake Solomoni, akamwuliza, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwanawe Hagithi, amejinyakulia mamlaka ya ufalme na bwana wetu Daudi hana habari? Basi, kama ukitaka kuyaokoa maisha yako na ya mwanao Solomoni, nakushauri hivi: Mwendee mfalme Daudi, umwulize, ‘Je, bwana wangu mfalme, hukuniapia mimi mtumishi wako ukisema, “Mwana wako Solomoni atatawala mahali pangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?” Imekuwaje basi, sasa Adoniya anatawala?’ Na utakapokuwa bado unaongea na mfalme, mimi nitaingia na kuyathibitisha maneno yako.” Basi, Bathsheba alimwendea mfalme chumbani mwake (wakati huo mfalme alikuwa mzee sana, naye Abishagi, Mshunami alikuwa akimhudumia). Bathsheba aliinama, akamsujudia mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Unataka nini?” Bathsheba akamjibu, “Bwana wangu, uliniapia mimi mtumishi wako mbele ya Bwana Mungu wako, ukisema: ‘Mwana wako Solomoni atatawala baada yangu, na ataketi juu ya kiti changu cha enzi.’ Sasa, tazama, Adoniya anatawala ingawa wewe bwana wangu mfalme hujui kuhusu hayo. Ametoa sadaka ya ng'ombe, ya vinono, na kondoo wengi, na kuwaita wana wote wa mfalme, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini mtumishi wako Solomoni hakumkaribisha. Na sasa, bwana wangu mfalme, Waisraeli wote wanakungojea, ili uwaambie yule atakayeketi juu ya kiti chako baada yako, bwana wangu mfalme. La sivyo, itatokea ya kwamba, wakati ambapo wewe bwana wangu, mfalme, utakapofariki mimi pamoja na mwanangu Solomoni tutahesabika kama wenye hatia.”