1 Wakorintho 7:25-35
1 Wakorintho 7:25-35 BHN
Sasa, kuhusu mabikira na waseja, sina amri kutoka kwa Bwana; lakini natoa maoni yangu mimi ambaye kwa huruma yake Bwana nastahili kuaminiwa. Basi, kutokana na shida iliyopo sasa nadhani ingefaa mtu abaki kama alivyo. Je, umeoa? Basi, usitake kuachana na mkeo. Wewe hukuoa? Basi, usitake kuoa. Lakini ikiwa utaoa hutakuwa umetenda dhambi; na msichana akiolewa hatakuwa ametenda dhambi. Hao watakaooana watapatwa na matatizo ya dunia hii, lakini mimi ningependa hayo yasiwapate nyinyi. Ndugu, nataka kusema hivi: Muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa na waishi kama vile hawakuoa; wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu; nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu, kama tuujuavyo, unapita. Ningependa nyinyi msiwe na wasiwasi. Mtu asiye na mke hujishughulisha na kazi ya Bwana jinsi atakavyompendeza Bwana. Mwanamume aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia jinsi atakavyompendeza mkewe, naye amegawanyika. Mwanamke asiyeolewa au bikira hujishughulisha na mambo ya Bwana apate kujitolea mwili na roho kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii jinsi atakavyompendeza mumewe. Nawaambieni haya kwa faida yenu, na si kwa kuwawekeeni kizuizi. Nataka tu muwe na mpango unaofaa, mpate kumtumikia Bwana kwa moyo na nia moja.