Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 21

21
Yesu anatokea wanafunzi saba.
1Kisha Yesu akajijulisha tena kwa wanafunzi kwenye bahari ya Tiberia. Alivyojijulisha ni hivyo: 2walikuwako pamoja Simoni Petero na Toma anayeitwa Pacha na Natanaeli wa Kana wa Galilea na wana wa Zebedeo na wanafunzi wake wengine wawili.#Yoh. 1:45. 3Simoni Petero alipowaambia: Nakwenda kuvua, wakamwambia: Nasi tunakwenda pamoja na wewe. Basi, wakaondoka, wakaingia chomboni, lakini usiku ule hawakupata kitu. 4Kulipoanza kucha, Yesu alikuwa amesimama ufukoni, lakini wanafunzi hawakumjua, ya kuwa ndiye Yesu.#Yoh. 20:14; Luk. 24:16. 5Yesu alipowauliza: Wanangu, hamna kitoweo? wakamjibu: Hatuna.#Luk. 24:41. 6Ndipo, alipowaambia: Utupeni wavu kuumeni kwa chombo, ndiko, mtakakopata! Walipoutupa, tena hawakuweza kuuvuta kwa ajili ya samaki wengi.#Luk. 5:4-7. 7Ndipo, yule mwanafunzi, Yesu aliyempenda, alipomwambia Petero: Ni Bwana! Simoni Petero aliposikia, ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi, kwani alikuwa uchi, akajitupa baharini.#Yoh. 13:23. 8Wanafunzi wenziwe wakaenda kwa chombo wakiuvuta wavu uliojaa samaki, kwani pwani hapakuwapo mbali, palikuwa kama mikono 200 tu. 9Nao waliposhuka pwani wakaona: moto wa makaa ulikuwa umewashwa, navyo visamaki vilikuwa vimewekwa juu pamoja na mkate. 10Yesu akawaambia: Leteni kidogo katika visamaki hivyo, mlivyovivua sasa hivi! 11Simoni Petero akapanda chomboni, akauvuta wavu ufukoni; wakawamo samaki wakubwa tu 153. Nao wavu haukupasuka, wangawa wengi kama hao. 12Kisha Yesu akawaambia: Njoni, mle! Miongoni mwao hao wanafunzi hakuwamo hata mmoja aliyejipa moyo wa kumwuliza: Wewe u nani? Walimjua, ya kuwa ndiye Bwana. 13Kisha Yesu akaenda, akautwaa mkate, akawagawia, na kitoweo vilevile.#Yoh. 6:11. 14Hii ndiyo mara ya tatu, Yesu akijijulisha kwa wanafunzi alipokwisha fufuka katika wafu.
Yesu na Petero.
15*Walipokwisha kula, Yesu akamwuliza Simoni Petero: Simoni wa Yohana, wanipenda kuliko hawa? Akamwambia: Ndio, Bwana, wewe unajua, ya kuwa ninakupenda. Akamwambia: Walishe wana kondoo wangu!#Yoh. 1:42. 16Alipomwuliza tena mara ya pili: Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia: Ndio, Bwana, wewe unajua, ya kuwa ninakupenda. Akamwambia: Vichunge vikondoo vyangu!#1 Petr. 5:2,4. 17Alipomwuliza mara ya tatu: Simoni wa Yohana, Wanipenda? Petero akasikitika, kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: Wanipenda? akamwambia: Bwana, wewe unayajua yote, wewe unatambua, ya kuwa ninakupenda. Yesu akamwambia: Vilishe vikondoo vyangu!#Yoh. 13:38; 16:30. 18Kweli kweli nakuambia: Ulipokuwa kijana ulijifunga mwenyewe, ukaenda, ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utainyosha mikono yako, mwingine akuvike, akupeleke, usikotaka. 19Neno hili alilisema, amwonyeshe kufa, alikotakiwa, amtukuze Mungu nako. Alipokwisha kuyasema haya akamwambia; Nifuate!*#Yoh. 13:36. 20Petero alipogeuka akaona, anafuata naye yule mwanafunzi, Yesu aliyempenda, ni yule aliyekuwa ameegamia kifuani pake, walipokuwa wakila jioni, aliyemwuliza: Bwana, ni nani, atakayekuchongea?#Yoh. 13:23. 21Basi, Petero alipomwona huyu akamwuliza Yesu: Bwana, na huyu je? 22Yesu akamwambia: Nikitaka, huyu akae, mpaka nitakapokuja, wewe unavikataliaje? Wewe nifuate tu! 23Basi, neno hili likaenea katika ndugu la kwamba: Mwanafunzi huyu hatakufa. Lakini Yesu hakumwambia: Hatakufa, ila: Nikitaka, huyu akae, mpaka nitakapokuja, wewe unavikataliaje?
24Huyu ndiye mwanafunzi aliyeyashuhudia haya na kuyaandika. Nasi twamjua, ya kuwa ushuhuda wake ni wa kweli.#Yoh. 15:27. 25Lakini yako hata mengine mengi, Yesu aliyoyafanya. Nayo kama yangaliandikwa moja moja, nadhani, ulimwengu wote usingevitoshea vitabu vitakavyoandikwa.#Yoh. 20:30.

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 21: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia