Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 19

19
Kilemba cha miiba.
1Ndipo, Pilato alipomchukua Yesu, akampiga viboko. 2Kisha askari wakasuka kilemba cha miiba, wakamvika kichwani, wakamvika hata nguo ya kifalme, 3wakamjia wakisema: Pongezi, mfalme wa Wayuda! wakampiga makofi. 4Pilato alipotoka tena nje, akawaambia: Tazameni, ninampeleka kwenu nje, mpate kutambua, ya kuwa sioni kwake neno la kumhukumu. 5Yesu akatoka nje, amekivaa kilemba cha miiba na nguo ya kifalme. Pilato akawaambia: Mtazameni mtu huyu! 6Watambikaji wakuu na watumishi walipomwona wakapiga makelele wakisema: Mwambe msalabani! Mwambe msalabani! Pilato alipowaambia: Mchukueni ninyi, mmwambe msalabani! Kwani mimi sioni kwake neno la kumhukumu. 7Wayuda wakamjibu: Sisi tuko na Maonyo, kwa Maonyo hayo sharti afe, kwani amejifanya kuwa Mwana wa Mungu.#Yoh. 10:33; 3 Mose 24:16. 8Pilato alipolisikia neno hili akakaza kuogopa, 9akaingia tena bomani, akamwuliza Yesu: Umetoka wapi? Lakini Yesu hakumjibu neno. 10Pilato alipomwambia: Husemi na mimi? Hujui, ya kuwa nina nguvu ya kukufungua na nguvu ya kukuwamba msalabani? 11Yesu akajibu: Hungekuwa na nguvu ya kunihukumu, kama usingepewa toka juu. Kwa hiyo yule aliyenitia mikononi mwako yuko na kosa linalolipita lako. 12Toka hapo Pilato alitafuta njia ya kumfungua. Lakini Wayuda wakapiga makelele wakisema: Unapomfungua huyu hu mpenzi wake Kaisari. Kila mwenye kujifanya kuwa mfalme humkataa Kaisari.
Kuhukumiwa kwake Yesu.
13Pilato alipoyasikia maneno haya akampeleka Yesu nje, akaketi katika kiti cha uamuzi mahali panapoitwa Kiwanja cha Mawe, lakini Kiebureo: Gabata. 14Lakini ilikuwa siku ya kuandalia Pasaka kama saa sita; alipowaambia Wayuda: Mtazameni mfalme wenu! 15wale wakapiga makelele: Mwondoe! Mwondoe! Mwambe msalabani! Pilato alipowaambia: Nimwambe mfalme wenu msalabani? watambikaji wakuu wakajibu: Hatuna mfalme pasipo Kaisari.#Yoh. 19:6.
(6-30: Mat. 27:31-50; Mar. 15:20-37; Luk. 23:26-46.)
16Basi, hapo ndipo, alipomtoa, awambwe msalabani.
I.N.R.I.
Wakampeleka Yesu; 17naye akajichukulia mwenyewe msalaba wake alipotoka kwenda mahali panapoitwa Fuvu la Kichwa, jina lake Kiebureo: Golgota. 18Ndipo, walipomwamba msalabani; tena pamoja naye wakawamba misalabani wengine wawili, huku na huko, lakini Yesu katikati. 19Pilato akaandika mwandiko, akaubandika msalabani juu; hapo palikuwa pameandikwa: YESU WA NASARETI, MFALME WA WAYUDA. 20Mwandiko huo Wayuda wengi waliusoma, kwani mahali pale, Yesu alipowambwa msalabani, palikuwa karibu na mji. Nao ulikuwa umeandikwa Kiebureo na Kiroma na Kigriki. 21Watambikaji wakuu wa Wayuda walipomwambia Pilato: Usiandike: Mfalme wa Wayuda, ila: Huyu amesema: Mimi ni mfalme wa Wayuda! 22Pilato akajibu: Niliyoyaandika, basi, nimekwisha kuyaandika.
Nguo za Yesu.
23Askari walipokwisha kumwamba Yesu msalabani wakayachukua mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kila askari fungu moja, wakaichukua hata kanzu. Lakini ile kanzu ilikuwa pasipo mshono, toka juu yote ilikuwa imefumwa tu. 24Kwa hiyo wakaambiana: Tusiipasue, ila tuipigie kura, ajulike atakayeipata. Imekuwa hivyo, litimie lililoandikwa:
Wakajigawanyia nguo zangu,
nalo vazi langu zuri wakalipigia kura.
Ndio askari waliofanya hivyo.#Sh. 22:19.
Yohana na Maria.
25Lakini penye msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama akina mama yake na ndugu ya mama yake, jina lake Maria wa Klofa, na Maria Magadalene. 26Yesu alipomwona mama yake na yule mwanafunzi, aliyempenda, akisimama karibu, akamwambia mama yake: Mama, tazama, mwana wako huyu!#Yoh. 13:23. 27Kisha akamwambia yule mwanafunzi: Tazama, mama yako huyu! Tokea saa ileile yule mwanafunzi akamchukua, akampeleka nyumbani mwake.
Kufa kwake Yesu.
28Baadaye Yesu alipojua, ya kuwa yote yamekwisha timizwa, akasema: Nina kiu, kwamba nayo hayo yaliyoandikwa yapate kutimia.#Yoh. 13:3; 18:4; Sh. 22:16. 29Palikuwa pamewekwa chombo kilichojaa siki. Basi, wakachukua mwani, wakauchovya sikini, wakautia katika kivumbasi, wakampelekea kinywani.#Sh. 69:22. 30Yesu alipokwisha pewa ile siki, akasema: Yamemalizika. Kisha akainama kichwa, akakata roho.
Donda la ubavuni.
31Kwa Wayuda siku ile ilikuwa ya kuandalia Pasaka, kwa hiyo wakamwomba Pilato, miguu yao waliowambwa misalabani ivunjwe, waondolewe, miili yao isikae misalabani siku ya mapumziko, kwani siku ile ya mapumziko ilikuwa kuu.#Yoh. 19:14; 3 Mose 23:5-8; 5 Mose 21:23. 32Wakaja askari, wakawavunja miguu wa kwanza na wa pili, waliowambwa misalabani pamoja naye. 33Lakini walipofika kwa Yesu, wakiona, ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; 34ila askari mmoja akamchoma mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji. 35Yeye aliyeyaona hayo ameyashuhudia, nao ushuhuda wake ni wa kweli, naye anajua, ya kuwa anasema kweli, nanyi mpate kuyasadiki. 36Kwani hayo yalikuwa, yatimie yaliyoandikwa: Hakuna mfupa wake utakaovunjwa.#2 Mose 12:46; Sh. 34:21. 37Tena liko neno jingine lililoandikwa la kwamba: Watamtazama yule, waliyemchoma.#Zak. 12:10; Ufu. 1:7.
Kumzika Yesu.
(38-42: Mat. 27:57-61; Mar. 15:42-47; Luk. 23:50-55.)
38Hayo yalipokwisha, akatokea Yosefu wa Arimatia aliyekuwa mwanafunzi wa Yesu, lakini alikuwa amejifichaficha kwa kuwaogopa Wayuda; yeye ndiye aliyemwomba Pilato ruhusa ya kuuondoa mwili wa Yesu. Pilato alipompa ruhusa, akaenda, akauondoa mwili wake. 39Pakaja Nikodemo naye, ni yule aliyemjia usiku hapo kwanza, akaleta manemane iliyochanganyika na uvumba, yapata kama mizigo miwili.#Yoh. 3:2; Mat. 2:11. 40Kisha wakautwaa mwili wa Yesu, wakaufunga kwa sanda pamoja na yale manukato, kama Wayuda walivyozoea kuzika. 41Mahali pale, alipowambwa msalabani palikuwa na kiunga, namo mle kiungani mlikuwa na kaburi jipya, ambalo hajazikwa mtu bado ndani yake. 42Kwa sababu ni siku ya kuandalia kwa Wayuda, wakamweka Yesu mle, kwani lile kaburi lilikuwa karibu.

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 19: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia