Matendo ya Mitume 4
4
Petero na Yohana mbele ya wakuu.
1*Walipokuwa wakisema na watu, wakawajia watambikaji na mlinda Patakatifu na Masadukeo.#Luk. 22:4,52. 2Kwani walikasirika, kwa sababu walifundisha watu na kuwapigia mbiu ya kwamba: Wafu watafufuka kwa hivyo, Yesu alivyofufuka.#Tume. 23:8. 3Kwa hiyo wakawakamata, wakawatia kifungoni, mpaka asubuhi yake, kwani ilikuwa jioni. 4Lakini waliolisikia lile neno wengi wakalitegemea, waume tu wakawa kama 5000.#Tume. 2:47.
5Kulipokucha, wakakusanyika Yerusalemu wakubwa wao na wazee na waandishi 6na mtambikaji mkuu Ana na Kayafa na Yohana na Alekisandro nao wote waliokuwa wa ukoo wa mtambikaji mkuu. 7Kisha wakawasimamisha katikati, wakawauliza: Hilo ninyi mmelifanya kwa nguvu ya nani au kwa jina la nani?#Mat. 21:23. 8Ndipo, Petero alipojaa Roho takatifu, akawaambia: Nyie wakubwa wa watu wa kwetu na wazee,#Mat. 10:19-20. 9kwa kuwa mtu mwenye kilema amefanyiziwa vizuri, sisi twaulizwaulizwa leo: Huyu amepona kwa nguvu ya nani? 10Tambueni ninyi nyote na ukoo wote wa Isiraeli: Nguvu ya Jina la Yesu Kristo wa Nasareti, mliyemwamba msalabani ninyi, Mungu aliyemfufua katika wafu, hiyo nguvu yake ndiyo inayomsimamisha huyu mtu machoni penu, yuko mzima!#Tume. 3:6,13-16. 11Huyu ndiye lile jiwe lililokataliwa na ninyi waashi, lakini limekuwa jiwe la pembeni.#Sh. 118:22; Mat. 21:42. 12Tena hapana pengine panapopatikana wokovu, wala hapana Jina jingine chini ya mbingu, sisi watu tulilopewa, tuokoke nalo.*#Mat. 1:21. 13Walipomwona Petero na Yohana, walivyosema pasipo woga, tena ilipowaelea, ya kuwa ni watu wasiofundishwa wala Maandiko wala ujuzi wo wote, wakastaajabu, wakawatambua, ya kuwa walikuwa pamoja na Yesu. 14Lakini walipomtazama yule mtu aliyeponywa, anavyosimama pamoja nao, hawakuwa na neno la kujibu.#Tume. 3:8-9. 15Wakawaagiza, watoke barazani kwao wakuu kwenda nje, wakala njama wao kwa wao 16wakisema: Tuwafanyieje watu hawa? Kwani wamefanya kielekezo cha waziwazi kinachotambulikana kwa watu wote wakaao Yerusalemu; nasi hatuwezi kukikana.#Yoh. 11:47. 17Lakini kusudi isipate kuenea po pote kwa watu, tuwatishe, wasimwambie tena mtu ye yote jambo lo lote la Jina hilo.#Tume. 5:28. 18Kisha wakawaita, wakawakemea kabisa, wasiseme tena na kufundisha mambo ya Jina la Yesu. 19Lakini Petero na Yohana wakajibu wakiwaambia: Likateni shauri hilo wenyewe, kama inaongoka mbele ya Mungu, kuwasikia ninyi kuliko Mungu!#Tume. 5:29. 20Kwani sisi hatuwezi kuacha, tusiyaseme, tuliyoyaona nayo tuliyoyasikia. 21Lakini wakawatisha sana, wakawafungua, kwa sababu hawakuwaonea neno la kuwaumiza, kwa kuwa waliwaogopa watu. Kwani wote walimtukuza Mungu kwa yale yaliyofanyika, 22kwani yule mtu aliyefanyiwa kielekezo hivyo cha kuponywa, miaka yake ilipita 40.
Kuomba kwa Wakristo.
23Walipokwisha funguliwa wakaenda kwa watu wao, wakawasimulia yote, watambikaji wakuu na wazee waliyowaambia. 24Walipoyasikia, ndipo, wote pamoja walipompalizia Mungu sauti na kusema: Bwana, wewe ndiwe uliyezifanya mbingu na nchi na bahari navyo vyote vilivyomo! 25Uliisemesha Roho takatifu kwa kinywa cha mtoto wako Dawidi:
Mbona wamizimu hupiga makelele?#Sh. 2:1-2.
26Mbona makabila ya watu huwaza mambo yaliyo ya bure?
Wafalme wa nchi hushikana mioyo?
wakuu nao hula njama wakikaa pamoja,
wamkatae Bwana na Kristo wake.
27Hii ni kweli, kwani walikusanyika mjini humu, wamkamate mtoto wako mtakatifu Yesu, uliyempaka mafuta; akina Herode na Pontio Pilato walipatana na wamizimu na watu wa Isiraeli,#Luk. 23:12. 28wayafanye yote, uliyomtakia kale kwa mkono wako na kwa mapenzi yako, kwamba yatimie papo hapo.#Tume. 2:23. 29Na sasa, Bwana, yatazame matisho yao! Wape watumwa wako waliseme Neno lako waziwazi pasipo woga hata kidogo!#Ef. 6:19. 30Unyoshe mkono, uponye watu na kufanya vielekezo na vioja kwa Jina la mtoto wako mtakatifu Yesu! 31Walipoomba hivyo, hapo, walipokuwa wamekusanyika, pakatetemeka, wakajazwa wote Roho Mtakatifu, wakalisema Neno la Mungu waziwazi pasipo woga.
32*Nao wigi wa watu waliokuwa wamemtegemea Bwana, mioyo yao nazo roho zao zilikuwa moja; tena hakuwako hata mmoja aliyezitumia mali zake, kama ni zake mwenyewe, lakini vyote walivitumia bia.#Tume. 2:44. 33Nao mitume wakaushuhudia ufufuko wa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi, magawio makuu ya Mungu yakiwakalia wao wote.#Tume. 2:47. 34Kwa hiyo hakupatikana kwao aliyekosa vitu, alivyopaswa navyo. Kwani wote waliokuwa wenye mashamba au nyumba waliziuza,#Tume. 2:45. 35wakaziweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa, kama alivyokosa.* 36Kulikuwa na Mlawi aliyetoka Kipuro, jina lake Yosefu, aliyeitwa na mitume Barnaba, maana yake Mwana wa Tulizo,#Tume. 11:22,24. 37naye alikuwa na shamba, akaliuza, akazileta fedha, akaziweka miguuni pa mitume.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo ya Mitume 4: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.