Matendo ya Mitume 2
2
Kushuka kwake Roho Mtakatifu.
1Siku ya Pentekote (Hamsini) ilipotimia, wote walikuwa pamoja mahali palepale pamoja.#Tume. 1:14; 3 Mose 23:15-21. 2Mara kukatoka uvumi mbinguni kama wa upepo unaovuma na nguvu, ukaijaza nyumba yote, walimokuwa wakikaa. 3Tena zikaonekana ndimi zilizogawanyika kama za moto, zikawakalia kila mmoja wao.#Mat. 3:11. 4Wote wakajazwa Roho takatifu, wakaanza kusema kwa misemo mingine, kama Roho alivyowapa, watamke.#Tume. 10:44-46; 1 Kor. 14.
5Mle Yerusalemu walikuwamo wakikaa Wayuda wenye kumcha Mungu wa kila taifa lililoko chini ya mbingu.#Tume. 13:26. 6Ule mvumo uliposikilika, watu wengi wakakusanyika, wakashangaa, kwani kila mtu aliwasikia, wakisema msemo wake yeye. 7Wakastuka na kustaajabu wakisema: Kumbe hawa wote wanaosema sio Wagalilea! 8Tena inakuwaje, sisi kila mtu tukiisikia misemo ya kwetu sisi, tuliyozaliwa nayo? 9Sisi Waparti na Wamedi na Waelamu, nasi tunaokaa Mesopotamia na Yudea na Kapadokia, Ponto na Asia, 10Furigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia zinazoelekea Kirene, sisi Waroma tunaokaa ugenini huku, 11sisi tulio Wayuda nasi tulio wafuasi, Wakreta na Waarabu, twawasikia hawa, wakiyatangaza makuu yake Mungu kwa ndimi zetu! 12Wakastaajabu wote wakipotelewa nayo, wakaulizana wao kwa wao: Jambo hili litakwenda kuwaje? 13Lakini wengine wakafyoza wakisema: Wamelewa mvinyo mbichi!*
Mafundisho ya Petero.
14Ndipo, Petero alipoinuka pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake akawaambia: Nyie waume Wayuda nanyi nyote mnaokaa Yerusalemu, jambo hili sharti litambulike kwenu, mpate kuyasikiliza maneno yangu! 15Kwani hawa hawakulewa, kama ninyi mnavyowawazia, maana sasa ni saa tatu ya mchana. 16Lakini hili ndilo lililosemwa na mfumbuaji Yoeli, ya kuwa#Yoe. 2:28-32. 17Mungu anasema:
Siku za mwisho ndipo, itakapokuwa,
niwamiminie Roho yangu wote wenye miili ya kimtu.
Nao wana wenu wa kiume na wa kike watasema na kufumbua,
nao vijana wenu wataona maono;
nao wazee wenu wataoteshwa ndoto.
18Nao walio watumwa wangu waume na wake
nitawamiminia Roho yangu siku zilezile,
nao watasema na kufumbua.
19Nami nitafanya vioja juu mbinguni na vielekezo chini
katika nchi, vyenye damu na moto na moshimoshi.
20Jua litageuka, liwe giza, nao mwezi utageuka, uwe damu,
mbele ya kutimia kwake ile siku ya Bwana
iliyo kubwa, wanayoingoja wote.
21Tena itakuwa, kila atakayelitambikia Jina la Bwana, ataokoka.#Rom. 10:13.
22Enyi waume wa Kiisiraeli, yasikilizeni maneno haya! Yesu wa Nasareti alikuwa amejulikana, kwamba ametoka kwa Mungu hapo alipokuja kwenu na kufanya vya nguvu na vioja na vielekezo, tena ni Mungu aliyempa kuvifanya machoni penu, kama mnavyojua wenyewe. 23Kwa kuwa Mungu alikuwa amempatia kazi na kumkatia mpaka kwa vile, anavyovijua vyote, vikiwa havijatimia bado, kwa hiyo ametolewa, mkampata mikononi mwa wapotovu, mkamwua na kumwamba msalabani.#Tume. 4:28. 24Lakini Mungu akamfufua na kuufungua uchungu wa kufa, kwa sababu haikuwezekana, ashikwe kuzimuni.#Tume. 3:15. 25Kwani Dawidi anamsema:
Nalimwona Bwana mbele yangu kila, nilipokuwa,
kwani yuko kuumeni kwangu, nisitikisike.#Sh. 16:8-11.
26Kwa hiyo moyo wangu hufurahi,
nao ulimi wangu hushangilia;
hata mwili wangu utatulia kwa kuwa na kingojeo.
27Kwani hutaiacha roho yangu, ipotee kuzimuni,
wala hutamtoa akuchaye, apate kuoza kaburini.
28Unanitambulisha njia ziendazo penye uzima,
utanijaza furaha zilizopo usoni pako.
29Waume ndugu zangu, mnipe ruhusa, niseme kwenu waziwazi: Dawidi aliye babu yetu mkuu alikufa, akazikwa, nalo kaburi lake liko kwetu hata siku hii ya leo.#Tume. 13:36; 1 Fal. 2:10. 30Yeye kwa sababu alikuwa mfumbuaji, akajua, ya kuwa Mungu amemwapia kiapo, kwamba atatawalisha kitini pake mmoja aliye mzao wa kiunoni mwake.#2 Sam. 7:12-13; Sh. 89:4-5. 31Hayo aliyaona mbele, yakingali nyuma bado, akayasema na kuuelekea ufufuko wake Kristo, kwani hakuachwa kuzimuni, wala mwili wake haukupata kuoza. 32Huyo Yesu Mungu amemfufua, nasi sote tu mashahidi wake. 33Naye alipokwisha kupazwa juu, akae kuumeni kwa Mungu, akapata ruhusa kwa Baba yake kukitimiza kiagio cha Roho Mtakatifu, akaimimina yiyo hiyo, ninyi mnayoiona, tena mnayoisikia. 34Kwani Dawidi hakupaa mbinguni, lakini anasema mwenyewe:#Sh. 110:1.
35Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti kuumeni kwangu,
mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako!
36Kwa hiyo wote walio wa mlango wa Israeli watambue kweli: Huyo Yesu, mliyemwamba msalabani ninyi, Mungu amemfanya, awe Bwana na Kristo!#Tume. 5:31.
37Walipoyasikia haya wakachomwa mioyoni, wakamwambia Petero na mitume wengine: Waume ndugu zetu, tufanyeje?#Tume. 16:30. 38Petero akawajibu: Juteni, kila mmoja abatiziwe Jina lake Yesu Kristo, mwondolewe makosa yenu! Nanyi mkipate kipaji cha Roho Mtakatifu!#Tume. 3:17-19; Luk. 24:47. 39Kwani kiagio kile ni chenu ninyi na cha watoto wenu nacho chao wote walioko mbali, Bwana Mungu wetu atakaowaita, wamjie.#Yoe. 2:32. 40Sharti mwokolewe katika kizazi hiki kipotovu!#5 Mose 32:5; Fil. 2:15. 41Basi, waliolipokea neno lake, wakabatizwa; hivyo siku ile waligeuzwa kuwa wanafunzi watu wapata 3000. 42Wakaongozana na kuyashika mafundisho ya mitume, wakafanya bia ya kumegeana mkate na kuombeana kwa Mungu.#Tume. 20:7. 43Wote wakaingiwa na woga mioyoni mwao, kwani vioja na vielekezo vilivyofanywa na mitume vilikuwa vingi. 44Wao wote waliomtegemea Bwana walikuwa pamoja, navyo vyote wakavifanyia bia.#Tume. 4:32. 45Wakauza mali zao navyo vyote, walivyokuwa navyo, wakavigawia wote, kila mtu apate, kama alivyokosa. 46Kwa sababu mioyo yao ilikuwa mmoja tu, walikuwa pamoja kila siku hapo Patakatifu, wakamegeana mkate nyumba kwa nyumba wakipokea vyakula na kushangilia katika mioyo yao iliyowang'aa.#Tume. 2:42. 47Wakamsifu Mungu, wakawapendeza watu wote. Naye Bwana akawaongeza kila siku na kutia papo hapo wenye kuokoka.#Tume. 4:4; 5:14; 11:21; 14:1.
Iliyochaguliwa sasa
Matendo ya Mitume 2: SRB37
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.