Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 5

5
Huduma ya Isa huko Galilaya, na upinzani uliomkabili huko Yerusalemu
(Yohana 5:1–10:42)
Isa amponya mtu kwenye Bwawa la Bethzatha
1Baada ya haya, kulikuwa na Sikukuu ya Wayahudi, naye Isa akapanda kwenda Yerusalemu. 2Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa Bethzatha#5:2 maana yake Nyumba ya mizeituni; mahali pengine limetajwa kama Bethesda kwa Kiaramu, yaani Nyumba ya huruma, na pengine kama Bethsaida, yaani Nyumba ya uvuvi kwa Kiebrania, ambalo lilikuwa limezungukwa na makumbi matano. 3Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani vipofu, viwete, na waliopooza [wakingojea maji yatibuliwe. 4Kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji. Yule angekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao]#5:3-4 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.. 5Mtu mmoja aliyekuwa ameugua kwa miaka thelathini na nane alikuwa hapo. 6Isa alipomwona akiwa amelala hapo, na akijua amekuwa katika hali hiyo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?”
7Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana#5:7 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida., mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.”
8Isa akamwambia, “Inuka! Chukua mkeka wako na uende.” 9Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea.
Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato. 10Kwa hiyo viongozi wa Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato; si halali wewe kubeba mkeka wako.”
11Yeye akawajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Chukua mkeka wako na uende.’ ”
12Wakamuuliza, “Ni mtu gani huyo aliyekuambia uchukue mkeka wako uende?”
13Basi yule mtu aliyeponywa hakufahamu ni nani aliyemponya, kwa sababu Isa alikuwa amepotea ndani ya umati ule wa watu waliokuwa hapo.
14Baadaye Isa akamkuta yule mtu aliyemponya ndani ya Hekalu na kumwambia, “Tazama umeponywa. Usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo baya zaidi.” 15Yule mtu akaenda, akawaambia wale viongozi wa Wayahudi kuwa ni Isa aliyemponya.
Uzima kupitia Mwana
16Kwa hiyo viongozi wa Wayahudi wakaanza kumsumbua Isa, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato. 17Isa akawajibu, “Baba#5:17 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.” 18Maneno haya yaliwaudhi sana viongozi wa Wayahudi. Wakajaribu kila njia wapate jinsi ya kumuua, kwani si kwamba alivunja Sabato tu, bali alikuwa akimwita Mungu Baba yake, hivyo kujifanya sawa na Mungu.
Mamlaka ya Mwana wa Mwenyezi Mungu
19Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lolote peke yake. Yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lolote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo. 20Baba ampenda Mwana na kumwonesha yale ambayo yeye Baba mwenyewe anayafanya, naye atamwonesha kazi kuu kuliko hizi ili mpate kushangaa. 21Hakika kama vile Baba awafufuavyo wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo Mwana huwapa uzima wale anaopenda. 22Wala Baba hamhukumu mtu yeyote, lakini hukumu yote amempa Mwana, 23ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeyote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma.
24“Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini na kuingia uzimani. 25Amin, amin nawaambia, saa yaja, nayo saa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu#5:25 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili., nao watakaoisikia watakuwa hai. 26Kama vile Baba alivyo na uzima ndani yake, vivyo hivyo amempa Mwana kuwa na uzima ndani yake. 27Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa yeye ni Mwana wa Adamu.
28“Msishangae kusikia haya, kwa maana saa inakuja ambapo wale walio makaburini wataisikia sauti yake, 29nao watatoka makaburini. Wale waliotenda mema watafufuka wapate uzima, nao wale waliotenda maovu watafufuka ili wahukumiwe.
30“Mimi siwezi kufanya jambo lolote peke yangu. Ninavyosikia ndivyo ninavyohukumu, nayo hukumu yangu ni ya haki kwa kuwa sitafuti kufanya mapenzi yangu mwenyewe, bali mapenzi yake yeye aliyenituma.
Shuhuda kuhusu Isa
31“Kama ningejishuhudia mimi mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. 32Lakini yuko mwingine anishuhudiaye, na ninajua kwamba ushuhuda wake ni wa kweli.
33“Mlituma wajumbe kwa Yahya, naye akaishuhudia kweli. 34Si kwamba naukubali ushuhuda wa mwanadamu; la, bali ninalitaja hili ili ninyi mpate kuokolewa. 35Yahya alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake.
36“Ninao ushuhuda mkuu kuliko ule wa Yahya. Kazi ambazo Baba amenituma nizikamilishe, naam, kazi hizi ninazofanya, zinashuhudia kuwa Baba amenituma. 37Naye Baba mwenyewe ameshuhudia juu yangu. Hamjapata kamwe kuisikia sauti yake wala kuona umbo lake, 38wala hamna neno lake ndani yenu, kwa sababu hamkumwamini yeye aliyetumwa naye. 39Ninyi mnachunguza Maandiko mkidhani ya kuwa ndani yake mna uzima wa milele. Maandiko haya ndio yanayonishuhudia mimi. 40Lakini mnakataa kuja kwangu ili mpate uzima.
41“Mimi sikubali kutukuzwa na wanadamu, 42lakini mimi ninawafahamu. Ninajua kwamba hamna upendo wa Mungu mioyoni mwenu. 43Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, nanyi hamnipokei. Lakini mtu mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea. 44Mnawezaje kuamini ikiwa mnapeana utukufu ninyi kwa ninyi, lakini hamfanyi bidii kupata utukufu unaotoka kwa Mungu?
45“Lakini msidhani kuwa mimi nitawashtaki mbele za Baba. Mshtaki wenu ni Musa, ambaye mmemwekea tumaini lenu. 46Kama mngemwamini Musa, mngeniamini na mimi, kwa maana aliandika habari zangu. 47Lakini ikiwa hamwamini aliyoandika Musa, mtaaminije ninayoyasema?”

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia