Yohana 13
13
Isa awanawisha wanafunzi wake miguu
1Sikukuu ya Pasaka ilikuwa imekaribia. Isa alijua kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba#13:1 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni; naam, aliwapenda hadi mwisho.
2Isa alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia wazo la kumsaliti Isa ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. 3Isa, akijua kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake, na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. 5Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.
6Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, “Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?”
7Isa akamjibu, “Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa.”
8Petro akamwambia, “La, wewe hutaninawisha miguu kamwe.”
Isa akamjibu, “Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami.”
9Ndipo Simoni Petro akajibu, “Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!”
10Isa akamjibu, “Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu.” 11Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi.
12Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi. Akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana’; hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri kwenu mkiyatenda.
18“Sisemi hivi kuhusu ninyi nyote. Ninawajua wale niliowachagua. Lakini ni kutimiza andiko lisemalo, ‘Yeye aliyekula chakula changu ameinua kisigino chake dhidi yangu.’#13:18 Zaburi 41:9
19“Ninawaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa Mimi ndiye. 20Amin, amin nawaambia, yeyote anayempokea yule niliyemtuma anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma mimi.”
Isa anatabiri kusalitiwa kwake
(Mathayo 26:20-25; Marko 14:17-21; Luka 22:21-23)
21Baada ya kusema haya, Isa alifadhaika sana moyoni, akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”
22Wanafunzi wake wakatazamana bila kujua kuwa alikuwa anamsema nani. 23Mmoja wa wanafunzi wake, ambaye Isa alimpenda sana, alikuwa ameegama kifuani mwa Isa. 24Simoni Petro akampungia mkono yule mwanafunzi, akamwambia, “Muulize anamaanisha nani.”
25Yule mwanafunzi akamwegemea Isa, akamuuliza, “Bwana, tuambie, ni nani?”
26Isa akajibu, “Ni yule nitakayempa hiki kipande cha mkate baada ya kukichovya kwenye bakuli.” Hivyo baada ya kukichovya kile kipande cha mkate, akampa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. 27Mara tu baada ya kukipokea kile kipande cha mkate, Shetani akamwingia.
Isa akamwambia Yuda, “Lile unalotaka kulitenda, litende haraka.” 28Hakuna hata mmoja wa wale waliokuwa wameketi naye mezani aliyeelewa kwa nini Isa alimwambia hivyo. 29Kwa kuwa Yuda alikuwa mtunza fedha, wengine walifikiri Isa alikuwa anamwambia akanunue vitu vilivyohitajika kwa ajili ya Sikukuu, au kuwapa maskini kitu. 30Mara tu baada ya kupokea ule mkate, Yuda akatoka nje. Wakati huo ulikuwa ni usiku.
Mafundisho ya mwisho ya Bwana Isa
(Yohana 13:31–17:26)
Isa atabiri kuwa Petro atamkana
(Mathayo 26:31-35; Marko 14:27-31; Luka 22:31-34)
31Baada ya Yuda kutoka nje, Isa akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe, naye atamtukuza mara moja.
33“Watoto wangu, mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo. Mtanitafuta, na kama vile nilivyowaambia Wayahudi, vivyo hivyo sasa nawaambia na ninyi: Niendako, ninyi hamwezi kuja.
34“Amri mpya nawapa: Mpendane. Kama mimi nilivyowapenda ninyi, vivyo hivyo nanyi mpendane. 35Mkipendana ninyi kwa ninyi kwa njia hii, watu wote watajua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.”
36Simoni Petro akamuuliza, “Bwana, unaenda wapi?”
Isa akamjibu, “Ninakoenda huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye.”
37Petro akamuuliza tena, “Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Mimi niko tayari kuutoa uhai wangu kwa ajili yako.”
38Isa akamjibu, “Je, ni kweli uko tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yangu? Amin, amin nakuambia, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 13: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.