Ufunuo 14:6-13
Ufunuo 14:6-13 SRUV
Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, akiwa na Injili ya milele, awahubirie hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji. Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake. Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-kondoo. Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake. Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu. Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.