Zaburi 73:1-20
Zaburi 73:1-20 SRUV
Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, Kwa hao walio safi mioyo yao. Nami miguu yangu ilikuwa karibu kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu kuteleza. Maana niliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki. Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na miili yao ina nguvu. Hawana taabu kama watu wengine, Wala hawapati mapigo kama wanadamu wenzao. Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Udhalimu huwavika kama nguo. Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao. Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu. Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutangatanga duniani. Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao. Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu? Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi. Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Na kunawa mikono yangu nisitende dhambi. Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi. Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako. Nami nilifikiri jinsi ya kufahamu hayo; Ikawa taabu machoni pangu; Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao. Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika. Namna gani wameangamizwa punde! Wakafutiliwa mbali kwa vitisho. Ee Bwana, wamekuwa kama ndoto wakati wa kuamka, Uondokapo utaidharau sanamu yao.