Zaburi 119:89-112
Zaburi 119:89-112 SRUV
Ee BWANA, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele. Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo imethibitika. Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako. Kama sheria yako isingalikuwa furaha yangu, Hapo ningalipotea katika mateso yangu. Hata milele sitayasahau maagizo yako, Maana kwa hayo umenihuisha. Mimi ni wako, uniokoe, Kwa maana nimejifunza mausia yako. Wasio haki wameniotea ili kunipoteza, Nitazitafakari shuhuda zako. Nimeona ukamilifu wote kuwa na mwisho, Bali amri yako haina kikomo. Sheria yako naipenda mno ajabu, Ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa. Maagizo yako hunitia hekima kuliko adui zangu, Kwa maana ninayo sikuzote. Ninazo akili kuliko waalimu wangu wote, Maana shuhuda zako ndizo nizifikirizo. Ninao ufahamu kuliko wazee, Kwa kuwa nimeyashika mausia yako. Nimeiepusha miguu yangu na kila njia mbaya, Ili nilitii neno lako. Sikuziacha hukumu zako, Maana Wewe mwenyewe umenifundisha. Mausia yako ni matamu sana kwangu, Kupita asali kinywani mwangu. Kwa mausia yako najipatia ufahamu, Ndiyo maana naichukia kila njia ya uongo. Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. Nimeapa nami nikathibitisha, Kuzishika hukumu zako za haki. Nimeteswa mno; Ee BWANA, unihuishe sawasawa na neno lako. Ee BWANA, uziridhie sadaka za kinywa changu, Na kunifundisha hukumu zako. Nafsi yangu imo mkononi mwangu daima, Lakini sheria yako sikuisahau. Watendao uovu wamenitegea mtego, Lakini sitoki katika njia ya mausia yako. Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele, Maana ndizo changamko la moyo wangu. Nimeuelekeza moyo wangu nizitende amri zako, Daima, naam, hata milele.