Marko 12:1-11
Marko 12:1-11 SRUV
Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalizungushia ua, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Na kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu. Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, bila chochote. Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia majeraha ya kichwa, wakamfanyia jeuri. Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua. Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu. Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu. Basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu?