Marko 11:12-23
Marko 11:12-23 SRUV
Siku iliyofuata walipokuwa wakitoka Bethania, aliona njaa. Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia. Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa; wala hakumruhusu mtu yeyote kupitia katika hekalu akiwa amebeba kitu. Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi. Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangazwa na mafundisho yake. Na kulipokuwa jioni alitoka mjini. Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani. Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka. Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu. Amin, nawaambia, yeyote atakayeuambia mlima huu, Ng'oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.